Fanya haya ukikutana na mwenza ‘uliyemmis’

Dar es Salaam. Dakika chache za mwanzo mnapokutana na mwenza wako baada ya kutengana kwa muda, hata kama si mrefu, zina umuhimu mkubwa katika kuimarisha au kudhoofisha uhusiano wenu. Huenda mwenza wako alikuwa kazini au safarini, na kwa muda huo ukawa ukimkosa au hata hisia hizo zikaanza kupoa.

Unapokutana naye tena iwe ni uwanja wa ndege, kituo cha basi au anapoingia nyumbani, ni muhimu kujiuliza: unafanya nini?

Unachokifanya katika muda huo mfupi kinaweza kujenga upya ukaribu wenu au kuanza kuudhoofisha taratibu. Ni uchaguzi wako, lakini unashauriwa kuzingatia mambo yafuatayo:

Kabla ya kukutana naye uso kwa uso, jiandae vizuri kiakili. Jenga mawazo chanya kuhusu mwenza wako na epuka kuwaza mambo ya lawama au malalamiko.

Wapo ambao hukurupuka kuuliza zawadi mara tu mwenza anapowasili; hali hii mara nyingi huibua mvutano usio wa lazima.

Badala yake, panga jambo la kumfurahisha au njia ya kumpokea kwa upendo. Unaweza hata kuwasiliana naye mapema kujua muda wa kuwasili ili ujipange vizuri.

Dakika ya kwanza mnapotazamana inaweza kuathiri siku yenu nzima. Mwonekano wako iwe ni tabasamu, usafi wa mwili au harufu, unaweza kumvutia au kumkera mwenza wako. Ni muhimu kujali mwonekano wako, ikiwa ni pamoja na nywele, meno, ngozi na mavazi.

 Hili linawahusu wanawake na wanaume pia. Kuwa nadhifu na mwenye mvuto ni njia mojawapo ya kuonyesha unavyojithamini na kumheshimu mwenza wako.

Mpokee kwa tabasamu la upendo

Tabasamu lina nguvu kubwa kuliko maneno mengi. Linaweza kuwasilisha upendo, furaha na kuthamini uwepo wa mwenza wako. Mpokee kwa tabasamu linaloonyesha kuwa ni wa muhimu kwako.

Hata kama haujisikii kutabasamu, jitahidi kuonyesha hisia chanya, hasa katika dakika za mwanzo, kwani hali hii inaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa mawasiliano yenu.

Salimianeni kwa ukaribu wa kimwili

Kukumbatiana, kubusiana au kushikana mikono ni ishara muhimu ya ukaribu. Wengi hupenda kupokelewa kwa namna hii wanapowasili nyumbani au mahali fulani.

Kama kubusu si sehemu ya mazoea yenu, tafuteni njia nyingine ya kugusana kimwili, kama kushikana mikono au kumshika bega mwenza wako. Mgusano wa mwili una nafasi kubwa katika kuimarisha hisia za mapenzi.

Tengeneza mazingira ya utulivu

Baada ya kukutana, ni vyema kupeana muda wa kupumzika kabla ya kuanza mazungumzo mazito. Watu wengi wanaotoka kazini au safarini huhitaji muda wa kutuliza akili na miili yao.

Baadhi huhitaji dakika chache za ukimya, kusikiliza muziki au kujinyoosha, huku wengine wakipendelea kuanza kwa mazungumzo mepesi au kucheza na watoto. Ni muhimu kuelewana kuhusu mahitaji haya ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.

Kwa ujumla, namna unavyompokea mwenza wako baada ya muda wa kutengana,  ina mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa uhusiano wenu. Chagua vitendo vinavyojenga upendo, heshima na maelewano ya kudumu.