ZAIDI ya wanamichezo 5000 wanatarajia kukutana jijini Mbeya kwa ajili ya kushiriki michuamo ya Shirikisho la Michezo kwa Serikali za Mitaa Tanzania (Shimisemita) itakayoanza Agosti 15 hadi 29 mwaka huu, huku wenyeji Jiji la Mbeya wakitamba kufanya vizuri.
Michuano hiyo inatarajia kushirikisha Halmashauri zote 184 hapa nchini na mwaka huu kitaifa itafanyika jijini Mbeya, huku ikitajwa kuwa kichocheo cha fursa kiuchumi na kutangaza vivutio.
Akizungumza jijini hapa, mwenyekiti wa michezo hiyo, Jeshi Lupembe, aliliambia Mwanaspoti kwa sasa maandalizi yanaendelea vyema na lengo lao ni kuweka hamasa, umoja na kujenga uhusiano kwa watumishi wa Halmashauri.
Amesema michuano hiyo pia itakuwa sehemu ya kuunga mkono harakati za Serikali katika kupokea mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, ambapo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi wenyeji sambamba na Kenya na Uganda.
“Tutapata nafasi ya kuona vivutio vilivyopo hapa Mbeya, ngoma za utamaduni, itasaidia watumishi kujenga miili yao kiafya, kudumisha uhusiano na Rais Samia Suluhu atakuwa mgeni rasmi kufunga michezo hii,” amesema Lupembe.
Kwa upande wake katibu wa michezo hiyo, Henry Kapella amesema michuano hiyo itahusisha michezo mbalimbali ikiwamo netiboli, kikapu, mpira wa mikono, mpira wa miguu na washindi wataondoka na zawadi.
“Kutakuwa na riadha, michezo ya ndani na washindi watapewa zawadi, tunazitaka timu husika ziwe na madaktari wenye ujuzi, tunashukuru tumepata ushirikiano kwa hapa Mbeya,” amesema Kapella.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justice Kijazi, amesema uwenyeji wa jiji hilo utachochea fursa za kiuchumi na kufungua milango kwa vijana katika kuonesha vipaji.
“Tuko tayari kuwapokea, hii ni fursa kibiashara na uchumi utapanda, urafiki utatengenezwa kupitia michezo hii, jiji letu ni salama, kila kitu kipo na miundombinu ya viwanja ni uhakika,” amesema Kijazi.
Ofisa Utamaduni wa jiji hilo, Nimwindael Daniel amesema uwenyeji wao utasaidia kutangaza vivutio vya utalii ambavyo kutokana na michezo hiyo itaweza kuamsha fursa mbalimbali.
“Uwenyeji wetu ni chachu kwa wafanyabiashara, niwaombe wajiandae kikamilifu kupokea wageni kupitia michezo hii, tunaamini tutabaki na uchumi na sisi tumejipanga kubeba ubingwa,” amesema Nimwindael
