Simba mambo magumu, Dabi ya Mzizima ikiisha bila mbabe

Katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam ndiko ulikopigwa mchezo wa dabi ya Mzizima iliozikutanisha Azam FC na Simba katika kampeni ya kusaka taji la Ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Katika mtanange huo mkali, ulianza kwa kasi sana timu zote zikishambuliana kabla ya Azam kuutawala mchezo zaidi katika kipindi hicho.

Matajiri hao wa Chamazi walitengeneza nafasi kadhaa lakini hawakuweza kuzitumia vyema hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kama ilivyokuwa kwa Azam ndivyo ilivyokuwa kwa wapinzani wao Simba katika kipindi cha pili ambapo walionekana kutengeneza baadhi ya nafasi pasipo mafanikio.

Licha ya timu zote kuondoka bila kuliona lango la mwenzake, lakini mchezo huo ulionesha radha ya dabi kutokana na kandanda safi la kiufundi waliloonesha miamba hao.

Golikipa wa Azam FC, Aishi Manula ndio ameibuka kuwa nyota wa mchezo huo baada ya kuonesha ubora kwa kuokoa michomo kadhaa ambayo ilikuwa hatari kwenye lango lake.

Mchezo wa leo ulikuwa wa mzunguko wa pili katika Ligi Kuu, Simba ikishindwa kutamba mbele ya Azam kwa mara nyingine, kwani katika mzunguko wa kwanza Matajiri hao wa Chamazi walishinda mabao 2-0.

Tangu msimu wa 2024/2025 Simba imepata ushindi katika mchezo mmoja tu na kuambulia sare mara mbili pamoja na vichapo viwili kutoka kwa wahoka mikate hao.

Simba wamesalia katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 35 mbele ya Azam ambao wapo katika nafasi ya tatu na pointi 33. Mchezo unaofuata Wekundu wa Msimbazi watakuwa na mechi ya kiporo dhidi ya TRA United ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Ligi hiyo itaendelea tena hapo kesho ambapo kutakuwa na mchezo mmoja utakaozikutanisha Coastal Union dhidi ya Mtibwa Sugar katika dimba la Mkwakwani, Tanga.