MUDA mchache baada ya leo Aprili 5, 2026 Singida Black Stars kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa TRA United katika mechi ya Ligi Kuu Bara, Walima Alizeti hao wamevunja benchi lote la ufundi.
Taarifa iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo, imesema umefikia uamuzi huo kufuatia mwenendo mbaya wa matokeo yasiyoridhisha katika kipindi cha hivi karibuni.
“Uongozi wa Klabu ya Singida Black Stars unatangaza rasmi kuvunjwa kwa benchi zima la ufundi la timu kuanzia leo, tarehe 05 Aprili 2026. Uamuzi huu umefikiwa kutokana na mwenendo mbaya wa timu kufuatia matokeo yasiyoridhisha katika kipindi cha hivi karibuni,” imesema taarifa hiyo na kuongeza.
“Klabu itatoa taarifa kuhusu benchi la ufundi la mpito wakati ikiendelea na maandalizi ya michezo ijayo.”
TRA ilikuwa mwenyeji wa mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo ilikuwa na ushindani wa aina yake.
Dakika ya kumi ya mchezo huo, TRA United ilipata bao la kwanza baada ya beki wa Singida, Abdallah Kheri Sebo kujifunga kabla ya Christopher Tebandeje kuongeza la pili dakika ya 40 kupitia mkwaju wa penalti.
Ni kama Singida hawakuwa na bahati kwani walipata faida ya mkwaju wa penalti baada ya beki wa TRA United, Chamoe Karaboue kuguusa mpira kwa mkono katikati ya eneo la hatari.
Baada ya mwamuzi Hans Mabena kuamuru mkwaju huo, kiungo mshambuliaji wa Singida, Lamine Jarjou alipiga nje na kuifanya Singida kumaliza mechi hiyo bila bao.
Kipigo hicho ni cha pili Singida inapokea msimu huu kutoka kwa TRA United baada ya awali ikiwa nyumbani kuchapwa mabao 3-1.
Singida kwenye mechi sita za hivi karibuni, imeshinda mbili dhidi ya Tanzania Prisons ikiifunga mabao 2-1 na Mbeya City ikiichapa 4-1.
Mechi nne imepoteza dhidi ya Simba kwa mabao 2-1, Yanga ikichapwa mabao 3-0, Azam (2-1) na leo ikipoteza dhidi ya TRA kwa mabao 2-0.
Licha ya kuwa na matokeo hayo, lakini timu hiyo imesalia nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 25, tofauti ya pointi moja na Pamba Jiji iliyopo nafasi ya tano.
