Aliyeua kutelekeza mwili kando ya barabara, kunyongwa

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songea, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Deo Ramadhani, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua Melania Christian na kuutelekeza mwili wake kando ya barabara ya Mahinya, Songera.

Mauaji hayo yalitokea Julai Mosi 2023, ambapo mwili huo ulikutwa ukiwa umefunikwa na kanga, katika Kijiji cha Mlilayoyo, Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma.

Hukumu hiyo imetolewa Machi 26, 2026 na Jaji Emmanuel Kawishe na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji Kawishe amesema baada ya kusikiliza kwa kina ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka pamoja na utetezi wa mshtakiwa, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote.

Katika usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa mashtaka uliwasilisha jumla ya mashahidi 15 pamoja na vielelezo mbalimbali ili kuthibitisha shtaka hilo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Deo Ramadhani alimuua Melania, Julai Mosi, 2023, baada ya kumshambulia akiwa shambani ambapo tukio hilo lilihusisha vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na kumbaka kabla na baada ya kumuua.

Katika mwenendo wa kesi hiyo, mashahidi tofauti waliieleza Mahakama mazingira ya tukio hilo. Ushahidi ulionyesha kuwa marehemu aliondoka nyumbani kwake kwenda shambani lakini hakurejea, jambo lililozua wasiwasi kwa familia yake.

Siku iliyofuata, mwili wake ulikutwa kando ya barabara ukiwa umefunikwa kwa kanga.

Shahidi wa nne ambaye ni mtoto wa marehemu, alidai siku ya tukio mama yao aliondoka kwenda shambani ila hakurejea na kuwa walisubiri hadi usiku wa manane wakaamua kulala.

Alisema siku iliyofuata aliondoka kumfuata mama yake shambani na akiwa njiani alikuta mwili wake   kando ya barabara na kuwa aliomba msaada kwa shahidi wa tano ambaye walisaidiana kuripoti polisi.

Shahidi wa sita ambaye ni daktari aliyeufanyia mwili uchunguzi alisema kuwa kulikuwa na jeraha la uti wa mgongo na kuwa marehemu alikuwa amenyongwa.

Shahidi wa 10 ambaye aliandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa na   kwa mlinzi wa amani, mshtakiwa alikiri kumbaka na kumuua mwanamke huyo, aliyekuwa akivuna mahindi ambapo alionyesha mahali alipomlaza kando ya barabara baada ya kumuua.

Aidha uchunguzi wa awali katika eneo la tukio ulionyesha dalili za mapambano pamoja na kupatikana kwa kielelezo muhimu ambacho ni nguo ya ndani iliyodaiwa kuwa ya marehemu.

Ofisa huyo wa polisi alieleza kuwa mshtakiwa alikiri kuhusika na tukio hilo pamoja na matukio mengine ya ubakaji na mauaji.

Katika utetezi wake, Deo alikanusha kuhusika na mauaji hayo, akidai kuwa alilazimishwa kukiri kosa hilo na maofisa wa polisi na kwamba hakuwa na uhusiano wowote na marehemu.

Aidha, alieleza kuwa hana elimu ya kusoma na kuandika hivyo alisaini nyaraka bila kujua kilichokuwa kimeandikwa.

Mahakama ilianza kwa kubainisha kuwa jukumu la upande wa mashtaka ni kuthibitisha shtaka la mauaji bila kuacha shaka yoyote yenye msingi.

Ilielezwa kuwa katika kesi hii hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja wa kumwona mshtakiwa akitekeleza tukio hilo, hivyo uamuzi ulitegemea ushahidi wa kimazingira.

Mahakama ilieleza kuwa ili ushahidi wa aina hiyo ukubalike, ni lazima uunde mlolongo kamili wa matukio unaoelekeza moja kwa moja kwenye hatia ya mshtakiwa bila uwezekano mwingine wa kuondoa hatia.

Katika kuchambua ushahidi, Mahakama ilibaini kuwa ingawa baadhi ya vielelezo kama nguo ya ndani havikuweza kuthibitishwa kisayansi kuwa mali ya marehemu, ushahidi mwingine uliwasilishwa uliendelea kuunganisha tukio na mshtakiwa.

Mahakama ilikubali kuwa ushahidi wa mashahidi mbalimbali kuhusu mahali ulipokutwa mwili wa marehemu na hali yake ulisaidia kuthibitisha mazingira ya tukio, ingawa haukutosha peke yake kumtia hatiani mshtakiwa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Kawishe alieleza kuwa hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa mshtakiwa alilazimishwa kutoa maelezo yake.

Mahakama ilisisitiza kuwa ingawa hakukuwa na shahidi wa moja kwa moja aliyemwona mshtakiwa akitekeleza mauaji hayo, ushahidi wa mazingira uliwasilishwa uliunda mlolongo kamili unaoonyesha wazi kuwa mshtakiwa ndiye aliyefanya kitendo hicho.

Katika uchambuzi wake, Mahakama ilieleza kuwa ushahidi wa kimazingira unaweza kutumika kumtia hatiani mshtakiwa iwapo utaonyesha mfululizo wa matukio usiovunjika unaoelekeza kwenye hatia yake bila kuacha nafasi ya shaka yoyote.

Baada ya kupitia ushahidi wote, Mahakama iliridhika kuwa upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka hilo bila shaka yoyote na kuwa mshtakiwa alikuwa na nia ovu na alitekeleza kitendo hicho kwa makusudi.

Mahakama ilihitimisha kwa kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kumkuta na hatia ya mauaji.