Barker ashtukia mchongo wa kuitibulia Yanga

JANA usiku Simba ilikuwa uwanjani ikipambana na Azam katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini ndani ya hesabu za mchezo huo kocha wa wekundu hao, Steve Barker, kuna kitu amekishtukia kuhusu kuwania ubingwa na haraka akawapa akili mpya mastaa wa kikosi hicho.

Msimamo wa Ligi Kuu Bara unaongozwa na Yanga yenye pointi 41 baada ya kucheza mechi 17, nyuma yake ilikuwa Simba na pointi 34 kabla ya kucheza na Azam iliyokuwa na pointi 32 ikishika nafasi ya tatu.

Yanga mbali na kuongoza kwa pointi, pia ndiyo timu iliyofunga mabao mengi ikiwa nayo 35, lakini pia ikiruhusu machache, yaani matatu tu. Kwa upande wa Simba, kabla ya jana ilikuwa imefunga mabao 26 na kuruhusu sita katika mechi 15 ilizocheza.

Kama Simba itazichanga vizuri karata zake katika mechi mbili ili kuwa sawa kimichezo na Yanga, basi itaachwa pointi moja, lakini bado kuna kipengele cha tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, ambacho ndicho Barker anawataka wachezaji wa kikosi chake kukiangalia kimahesabu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesema ligi ni ngumu, ambapo hakuna ambaye ana uhakika wa kuchukua ubingwa, na anawataka wachezaji wake kujipanga kubadilisha tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kati yao na vinara.

Barker amesema kwenye hesabu hizo, kitu muhimu ni kuanza kutumia kwa wingi nafasi za kufunga, ambapo licha ya kwamba wanatengeneza nyingi, lakini wanatumia chache.

“Hakuna timu ambayo unaweza kusema moja kwa moja kwamba itakuwa bingwa msimu huu, kila kitu kipo wazi sana, lolote linaweza kutokea. Kama unavyoona kuna timu iliyo juu yetu, tumekuwa tukipunguza sana tofauti ya pointi kati yetu na wao,” amesema Barker.

“Ukiacha pointi, lakini kuna tofauti nyingine ya mabao kati yetu na wao, yapo tisa sasa (kabla ya jana). Katika ligi ngumu kama hii mnayofukuzana ni lazima mkae tayari kwa mapambano yote, unaweza kukuta timu inapata ubingwa kwa tofauti ya mabao.

“Tutaendelea kuangalia mechi zetu, tunatakiwa kulazimika kubadilika kwa kutumia nafasi zaidi za kufunga, kwa kuwa tunazitengeneza nyingi. Unaweza kuangalia mchezo uliopita (dhidi ya Coastal Union), mpaka mapumziko tulikuwa tunaongoza mbili, lakini tungeweza kuwa na mabao mengi zaidi.

“Tunaongea na vijana kila wakati, tunatakiwa kuongeza umakini tunapokuwa ndani ya eneo la hatari. Bado kuna wakati tunafanya mambo kwa presha, haitakiwi kuwa hivi. Simba ni moja ya timu inayocheza mpira mzuri, tunatakiwa kuongeza ufanisi wa kutumia nafasi ili tusijiweke pabaya.”