KUANZIA sasa, Black Sailors inahitaji pointi tisa tu ili msimu ujao ishiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPLB) baada ya msimu huu kuwa na mwendo mzuri katika Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja.
Sailors ndiyo kinara katika msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja ikiwa na pointi 56, ikifuatiwa na Raskazone (52), kisha Kundemba (38), ikiwa kila timu imecheza mechi 21, zikibaki tisa kukamilisha msimu, ikiiacha timu ya tatu kwa tofauti ya pointi 18.
Kwa mujibu wa kanuni za ligi hiyo, timu mbili za juu kwenye msimamo zinapanda daraja Ligi Kuu Zanzibar, zikiungana na mbili zingine kutoka Pemba na kufanya jumla kuwa nne.
Sailors inahitaji pointi hizo tisa na kufikisha 65 ili kuwa na uhakika wa kucheza Ligi Kuu msimu ujao kutokana na Kundemba inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 38, ikishinda mechi zote tisa zilizobaki itamaliza msimu na 65.
Sailors pia ina wastani mzuri wa mabao ambayo tofauti yake na Kundemba ni 21 na imefunga 51 na kuruhusu 14, huku Kundemba ikifunga 43 na kuruhusu 27 na katika mechi hizo tisa, mbili itacheza dhidi ya Raskazone na Kundemba.
Kwa upande wa Raskazone ambayo ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 52, ili kucheza Ligi Kuu Zanzibar msimu ujao, inatakiwa ishinde mechi tano kati ya tisa ili kupanda daraja bila ya kusubiri matokeo ya wengine.
Hesabu zinaonesha, Raskazone ikishinda mechi tano, itafikisha pointi 67 ambazo Kundemba haiwezi kuzifikia hata akishinda zote tisa zilizobaki.
Kwa mantiki hiyo, Kundemba bado ina kibarua kizito cha kuhakikisha inapanda Ligi Kuu baada ya msimu wa 2025-2026 kushuka na nafasi yake kuchukuliwa na Polisi.
Mechi tisa zilizobaki, Sailors itavaana na ZAFSA, Muungano Rangers, Ujamaa, Raskazone, Kundemba, Inter Zanzibar, Paje Star, New City na Negro United.
Kwa upande Raskazone, imebakisha kucheza dhidi ya Kikungwi, Sebleni, Muungano Rangers, Black Sailors, Inter Zanzibar, Paje Star, Urafiki, BZL na Taifa Jang’ombe.
Kundemba yenyewe mechi zake tisa ni dhidi ya BZL, Taifa Jang’ombe, Zafsa, Ujamaa, Black Sailors, New City, Negro United, Sharp Boys na Kikungwi.
