KOCHA wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka amesema ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Geita Queens umetokana na mabadiliko makubwa ya kiufundi na kisaikolojia kwa wachezaji wake.
Chobanka alikiri awali timu hiyo haikuwa kwenye kiwango kizuri, lakini walijifunza kutokana na makosa ya nyuma hasa baada ya kufungwa bao 1-0 na Geita.
Amesema siyo kikosi hicho ni kibovu, bali walikosa mwanzo mzuri ambao uliwaathiri katika mechi zilizopita.
Kocha huyo alieleza mapumziko ya mwezi mmoja yalikuwa na faida kubwa kwani yaliwapa muda wa kujipanga upya na kurekebisha mapungufu yaliyoonekana.
“Siyo kwamba timu ilikuwa mbaya kivile, isipokuwa hatukuanza vizuri hivyo mpango wetu uko pale pale wa kuhakikisha pointi tatu zinasalia nyumbani kila mechi,” amesema Chobanka na kuongeza;
“Mapumziko yamesaidia, tulikuwa na hali mbaya lakini tuliongea na wachezaji wapush ili timu ibaki kwenye ligi ndio tumeanza.”
Akizungumzia mechi ijayo, Ceasiaa itakutana na Alliance, timu ambayo aliwahi kuifundisha, jambo linaloifanya mechi hiyo kuwa na presha ya aina yake.
“Ni mechi ya kujitafakari, mimi na Kocha Sultan Juma tunawajua Alliance, lakini nao watakuja kwa kutukamia kwa sababu wanatufahamu.”
