Chadema yavunja ukimya bei ya mafuta, yataka mambo manne

Dar es Salaam. Wakati huduma mbalimbali zikiendelea kuathirika kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa mapendekezo manne kuleta unafuu kwa wananchi katika huduma hiyo.

Mapendekezo hayo ni Serikali kuweka ruzuku kwenye mafuta, kutangaza mpango wa dharura wa upatikanaji wa huduma hiyo, kuwepo kwa utaratibu wa uagizaji wake na kudhibiti bei ili wananchi wawe na unafuu.

Chadema inatoa mapendekezo hayo takribani wiki moja tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya ya mafuta, ambapo bei ya lita moja ilipaa kutoka Sh2,864 hadi Sh3,820, na hadi Sh4,000 kulingana na mkoa.

Hata hiyo, Aprili mosi, mwaka huu wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2026/2027 bungeni, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli na mafuta mengine ili kuhakikisha bei zake zinaendelea kuwa himilivu.

Amesema Serikali itachukua hatua licha ya kuwepo kwa changamoto za kiusalama za kikanda na kimataifa, ikiwemo za Mashariki ya Kati zilizosababisha kupanda kwa bei ya huduma hiyo.

Akizungumza leo, Aprili 6, 2026, kupitia mitandao ya kijamii, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, amependekeza ili wananchi wawe na unafuu katika huduma ya mafuta ni lazima Serikali iondoe tozo zote kwenye lita moja ya mafuta.

“Jambo hilo liendane na uwekaji wa utaratibu wa uagizaji wa bei ya mafuta katika hali iliyopo sasa nchini. Jambo la pili, mamlaka itangaze mpango wa ahueni kwa wananchi kwa muda wa siku 60 hadi 90, kwa kutoa ruzuku ili kuwalinda wananchi hasa katika usafirishaji na kilimo,” amesema.

Mbali na hayo, Heche amependekeza uwepo wa mpango wa dharura kuzuia upandaji wa mafuta kugeuka kuwa bei isiyohimiliwa.

Pia, amesema kwa vile mamlaka ilitoa taarifa ya uwepo wa akiba ya mafuta kwa miezi mitatu, mamlaka zidhibiti bei kwa kipindi hicho, kwani huduma hiyo ilitangazwa kuwa na akiba ya kutosha kwa miezi mitatu zaidi.

Amesema hali iliyopo sio ya kuvumiliwa bali ni ya kuchukuliwa hatua, na kwa sasa hakuhitajiki maneno mengi kwani kupanda kwa mafuta kwa kiwango cha kuumiza wananchi ni uzembe.

“Ongezeko la gharama za mafuta linabadilisha bei za vyakula sokoni, nauli ya daladala, bei ya unga sokoni, na mzigo wa maisha kwa kila kaya ya Watanzania.

“Kwa Tanzania ya leo, mafuta yakipanda bei, nauli hupanda, na nauli ikipanda, chakula nayo hupanda, na biashara ndogo huumia, mapato hushuka na wananchi huingia kwenye maumivu makubwa. Hapa ndio mafuta hubadilika kutoka takwimu kuwa maumivu,” amesema.

Heche amedai chama hicho ndicho kinasema ukweli kwa wananchi, akisisitiza Serikali inapaswa kuwajali wananchi na kutatua kero zilizopo.

Amesema gharama ya kununua mafuta kwa lita ni Sh1,800 hadi Sh2,000, na usafirishaji hukadiriwa kuwa Sh150 kwa lita moja, jumla Sh2,100 kwa lita,  bei ambayo ndiyo mafuta yalipaswa kuuzwa nchini.

Kiwango hicho kutotumika, ametaja kiini ni wingi wa tozo zilizowekwa kwenye mafuta, akitaja tozo ya petroli Sh300, ushuru wa bidhaa, na kodi nyingine. Kwa kila Sh100 anayolipa mwananchi kwenye mafuta, Heche amesema Sh31 ni tozo na ushuru za ndani.

“Kwa lugha rahisi zaidi, mzigo mkubwa zaidi unaoweza kujadiliwa kisera upo kwenye kodi na tozo za ndani, na hapa ndio mjadala unapaswa kuwepo,” amesema.