BAADA ya kufanya kweli katika mchezo uliopita, Dodoma Jiji imesema kwa sasa inafikiria jinsi ya kuvuka mtego dhidi ya Simba ili kujitabiria makubwa na historia mpya katika Kombe la Shirikisho la CRDB.
Aprili 2 mwaka huu, Dodoma Jiji ikicheza katika ubora wake, iliifanyia kitu mbaya Fountain Gate kwa kuikanda mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara na kupanda nafasi ya saba kwa pointi 24 na michezo 18.
Baada ya mchezo huo, timu hiyo inatarajia kushuka uwanjani Aprili 12 mwaka huu kucheza dhidi ya Simba katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB, kuisaka robo fainali ya michuano hiyo.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah amesema licha ya malengo waliyonayo kwenye michuano hiyo, lakini kihunzi cha kuvuka kwa Wekundu hao ni mwiba kwao na wataingia uwanjani kwa mbinu tofauti.
Amesema anachoamini ni ubora wa nyota wake na anafahamu wazi nafasi watakazopata huenda zikawa ndogo ikilinganishwa na wenyeji, lakini watakuwa makini kudhibiti hatari zote.
“Tumewafuatilia sana tumeona ubora wao, tunayo malengo yetu ila tunafahamu ugumu dhidi ya wapinzani hao, tukivuka kihunzi hicho ndio tunaweza kutamba mwelekeo wetu rasmi,” amesema Josiah.
Kocha huyo wa zamani wa Biashara United na Tanzania Prisons, aliongeza kwa sasa anaridhishwa na kiwango cha nyota wake ndani ya Ligi Kuu akitamba hesabu ni kumaliza nafasi nzuri.
Alikiri ligi imekuwa ngumu haswa zinapobaki mechi chache kwani wanakutana na timu zinazopambana kukwepa kushuka daraja na kuwania ubingwa, hivyo benchi la ufundi linasoma mechi zote ili kufikia malengo.
“Huu ndio muda wa kupanga hesabu ili tumalize ligi bila presha, tunakutana na makundi mawili ya kushuka daraja na kuwania ubingwa, hivyo sisi tukimaliza nafasi tano hadi saba si mbaya,” amesema kocha huyo.
