FOUNTAIN Gate imesema tatizo la timu hiyo kutokuwa na matokeo mazuri ni kutokana na ufinyu wa kikosi chake na mechi nne zijazo ikiwamo dhidi ya Simba itakazocheza nyumbani ndizo zitaamua zaidi hatma yao.
Hata hivyo, imesisitiza mechi hizo dhidi ya Simba, Mtibwa Sugar, Dodoma Jiji na Coastal Union zitakuwa za kufa au kupona kuhakikisha hawapotezi hata pointi ili kuwasaidia kujinasua nafasi za mkiani.
Timu hiyo ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 16 kabla ya mechi ya jana na Aprili 12 mwaka huu inatarajiwa kuwa uwanjani kuikabili Azam FC kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB, kisha kurejea nyumbani kucheza mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Bara ikianza Aprili 15 mwaka huu dhidi ya Simba.
Meneja wa timu hiyo, Elias Zamkufo amesema kinachowakuta kwa sasa ni kutokana na ufinyu wa kikosi baada ya rungu la kutofanya usajili hadi kufikia hatua ya kuwatumia zaidi vijana chipukizi waliopandishwa kutoka U20.
Amesema pamoja na hali hiyo, wanaendelea kusuka mipango ya chini chini kuhakikisha timu haishuki daraja wala kucheza mchujo ‘play off’ ili msimu ujao watengeneze kikosi imara na chenye ushindani zaidi.
“Tunao wachezaji 19, wengine ni wale wa kujitafuta, lakini changamoto hiyo tumeshaiona na tunaifanyia kazi kuona ni namna gani tunatoboa kubaki salama Ligi Kuu, hatutaki kucheza play off wala kushuka daraja,” amesema Zamkufo.
Zamkufo aliyewahi kucheza Mbao FC na timu hiyo, ameongeza baada ya mchezo ujao dhidi ya Azam, wanahitaji kutumia michezo minne ya nyumbani wakianza na Simba kuhakikisha hawaachi kitu.
Amesema wanafahamu ugumu wa ligi na ubora wa timu pinzani lakini kwa sapoti na hamasa iliyopo kwa uongozi wao wanaamini watapata matokeo mazuri na timu kukwepa aibu ya kushuka daraja.
“Tunakumbuka yaliyotukuta msimu uliopita na ndio maana tunapambana yasijitokeze tena, kinachotupa nguvu ni sapoti na hamasa ya uongozi kupitia mkurugenzi namna anavyojali wachezaji,” amesema meneja huyo.
