Waumini wa Dayosisi ya Kibondo Kanisa Anglikana Tanzania, 6 aprili 2026, walijitokeza kwa wingi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Hilario – Kibondo, kushiriki Ibada ya Misa Takatifu maalumu ya Upatanisho na Msamaha.
Ibada hiyo maalumu iliongozwa na Askofu Daudi Ndahana, ili kuomba toba na msamaha kwa Mungu kufuatia mgogoro ulioibuka wakati wa uchaguzi wa kumpata Askofu wa pili wa Dayosisi hiyo, mwezi Septemba 2025 ambao uliwagawa waumini na baadhi kutengwa na Kanisa.
Askofu Ndahana alisema, mgogoro huo ulitengeneza hali ya tofauti kati ya waumini na Kanisa, hivyo uongozi ulifanya jitihada za kutafuta Suluhu kwa njia ya amani, kisha kuandaa Ibada ya upatanisho ambayo imetumika kuwapokea Wahudumu na waumini waliotengwa na huduma ya Kanisa.
“Tumekuja hapa ili kuomba Toba na Msamaha kwa Mungu, wakati wa mchakato wa uchaguzi wa uaskofu tulikosea, pia leo tumewarudisha kundini wenzetu waliotengwa na Kanisa” alisema Askofu Ndahana.
Kasisi Canon. Dkt. George Otieno Lawi, Katibu Mkuu Kanisa Anglikana Tanzania, alishiriki Ibada hiyo na kueleza kufurahishwa na hatua ya maridhiano iliyofikiwa na Dayosisi ya Kibondo ili kulinda afya ya Kanisa.
“Dayosisi ya Kibondo ilipita katika kipindi kigumu wakati wa mchakato wa kumpata Askofu wa pili, lakini Leo nina furaha kuona Kanisa limefikia hatua hii muhimu, Mungu awabariki sana” alisema Katibu Mkuu Lawi.
Wakizungumza kwa niaba ya waumini waliorudishwa kundini kuendelea na ushirika wa Kanisa katika Dayosisi ya Kibondo, James Ngomagi na Sedekia Ruduga, walisema, baada ya kutafakari kwa kina waliona ni vyema kujishusha ili kuliponya Kanisa la Mungu.
“Tulitofautiana na Kanisa la Mungu, baada ya kutafakari kwa kina Tukatafuta njia ya maridhiano Tunashukuru Mungu na Kanisa kutupokea” walisema.
Baadhi ya waumini walioshiriki Ibada hiyo akiwemo Bw. Zamoyoni Uzale, Lameck Kagina, Bi, Irene Ulimwengu na Jenipher Wilson walisema, Ibada hiyo imekuwa ya baraka na mafanikio kwa Kanisa la Mungu.
“Tumeshiriki Ibada ambayo imekuwa ya amani na furaha mbele za Mungu kwakuwa tumeona hatua ya upatanisho tunaamini haya ni mafanikio katika kukuza Injili ya Kristo” walisema waumini hao.
Ibada hiyo ilitanguliwa na zoezi la kuteketeza kwa moto fimbo na miti iliyotumiwa wakati wa vurugu za mchakato huo ili kuonesha kuwa jambo hilo limeisha na kuendelea kulitangaza jina la Mungu.




