ALICHOKIFANYA kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ msimu wa 2023-2024 na 2024-2025 na muendelezo wake msimu huu, kimewaibua baadhi ya mastaa wa zamani kuona anaweza akaandika rekodi ya aina yake.
Kitu kikubwa kilichowafurahisha mastaa hao ni data za Fei Toto ambapo msimu wa 2023-2024 alikuwa na mabao 19 huku akitoa asisti saba, wakati 2024-25 akifunga mabao manne na asisti 13 na msimu huu tayari ana mabao saba na asisti tano kabla ya mechi dhidi ya Simba.
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Nurdin Bakari, amesema endapo Fei Toto ataendelea kukomaa na wachezaji wenzake wa Azam wakamfanya ndiyo tegemeo kwa kumkabidhi mipira ya kufunga basi anaweza akaibuka mfungaji bora, ingawa hilo halina asilimia zote kwani bado mechi zimesalia nyingi.
“Natambua anayeongoza kwa mabao ni Ngoy (Fabrice) wa Namungo ana mabao manane, lakini nimeangalia muendelezo wa ufungaji unapishana muda gani,” amesema staa huyo na kuongeza;
“Fei anafunga na kutoa asisti, hilo linamuonyesha ni mtu anayepatikana maeneo mengi ya uwanja, lakini anafanya hivyo kila msimu ndiyo maana anawaniwa na kila timu ikitaka huduma yake, apambane anaweza akaandika rekodi mpya ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora.”
Kauli yake iliungwa mkono na nahodha wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi aliyesema: “Ingawa mchezaji yoyote anaweza akachukua kiatu cha ufungaji msimu huu, ila jambo la msingi waliyo na mabao mengi wanafunga kila baada ya muda gani, hiyo itakuwa silaha ama mbinu ya mtu kuibuka kinara dhidi ya wengine, kuhusu Fei ni nchezaji mwenye mchango mkubwa wa mabao Azam, asipofunga anatoa asisti.”
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Meddie Kagere amesema: “Fei ni kati ya wachezaji wenye vipaji na uwezo, akipambana na akawa na muendelezo wa kufunga sina shaka anaweza akafunga mabao mengi.”
Kabla ya mechi ya Azam dhidi ya Simba iliyopigwa jana, Fei kuanzia msimu wa 2023-2024, 2024-2025 na sasa 2025/26 katika Ligi Kuu Bara, jumla amefunga mabao 30 na asisti 25, hivyo amehusika katika mabao 55 tangu atue Azam akitokea Yanga.
