……
Na: Mwandishi Wetu, Pangani
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Bara na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Mussa Mwakitinya, amezindua rasmi mashindano ya mpira wa miguu yaliyopewa jina la “Aweso Vijana Cup,” wilayani Pangani mkoani Tanga.
Uzinduzi huo umefanyika Aprili 4, 2026, katika uwanja wa Kata ya Mwera. Katika hotuba yake fupi ya ufunguzi, Mwakitinya ameupongeza uongozi wa UVCCM wa wilayani humo kufuatilia uratibu mzuri wa mashindano hayo huku akisisitiza umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu ili kukuza vipaji vyao.
“Vijana wetu wana uwezo mkubwa, kupitia Aweso Vijana Cup tunafungua jukwaa la wao kuonyesha vipaji vyao na kujijengea mustakabali bora,” amesema Mwakitinya.
Sambamba na hilo, Mwakitinya amesema serikali ipo pamoja na wadau wote wa michezo ili kuhakikisha sekta ya michezo inakua na inachangia maendeleo ya nchi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Tanga, Ramadhani Omary, amesema vijana ni wadau muhimu kwa uhai wa Chama na maendeleo ya nchi, hivyo wanapaswa kutumia fursa zilizopo katika mazingira yao ikiwemo suala la michezo.
Katika mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo, timu ya Tungamaa ilipata ushindi wa (1-0) dhidi ya Mwera. Tungamaa ilipata goli la ushindi katika dakika 87, kupitia kwa mchezaji wake Said Mandera, na hivyo kuchukua alama tatu muhimu.
Mashindano hayo yanahusisha timu kutoka Kata zote 14 za wilaya ya Pangani huku mfadhili wa mashindano hayo akiwa ni Mbunge wa Jimbo la Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.



