Global Publishers
April 6, 2026
0 Comments
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Aprili 6, 2026 amekagua madhara yaliyosababishwa na ajali ya moto katika soko la wafanyabiashara wadogo la Simu 2000 lililopo Ubungo.
Moto huo ulitokea Aprili 4, 2026 na kusababisha uharibifu mkubwa, ambapo takribani vibanda 500 vya wafanyabiashara wadogo viliteketea kabisa, hali iliyowaacha wengi wakikosa mtaji na bidhaa zao.

Akizungumza baada ya kukagua eneo hilo, Waziri Mkuu alieleza masikitiko yake kwa wafanyabiashara walioathirika na kuwahakikishia kuwa Serikali itachukua hatua za haraka kusaidia kurejesha shughuli zao.
Aidha, aliwataka mamlaka husika kuchunguza chanzo cha moto huo ili kuepusha matukio kama hayo kujirudia, huku akisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuzingatia tahadhari za usalama dhidi ya majanga ya moto.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara waliopoteza mali zao walieleza kuwa wamepata hasara kubwa na kuiomba Serikali kuwasaidia ili waweze kurejea katika biashara zao haraka.
Tukio hilo limeibua hofu na huzuni kwa jamii ya eneo hilo, huku juhudi za kurejesha hali ya kawaida zikiendelea.
