WAKATI mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wakiwa hawajapoteza mechi katika ligi hiyo msimu huu, Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William amesema kikosi chao kinajipanga kuondoka na ushindi watakapokutana kesho Jumatano kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Akizungumzia mechi hiyo, William amesema kauli mbiu wanaoingia nayo ni “WANAFUNGIKA”, na amebainisha licha ya nafasi iliyopo Yanga kwenye msimamo ikiongoza, lakini hakuna inachowazuia Pamba Jiji kushinda.
“Kwa sababu wao ni kama sisi, wote tunaongozwa na sheri 17 za mpira wa miguu licha ya ubora na nafasi waliyopo, lakini tumetazama michezo yao na tunaamini kwa ubora wa timu tuliyonayo tunaweza kuwafunga,” amesema William.
Pamba Jiji itaingia uwanjani ikiwa imetoka kupata matokeo ya 0-0 ugenini dhidi ya Mashujaa, mchezo uliopigwa Aprili 4 mwaka huu kwenye Dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma, huku Yanga ikiichapa Tanzania Prisons mabao 3-0.
Timu hizo zilipokutana duru la kwanza, Yanga ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, huku pia msimu uliopita uwanjani hapo CCM Kirumba, wenyeji Pamba Jiji walilala kwa mabao 3-0 na msimu huo ugenini ikafungwa tena 4-0 na kufanya mechi tatu za kukutana kwao, Yanga ikishinda kwa jumla ya mabao 10-0.
Hata hivyo, msimu huu Pamba Jiji ni miongoni mwa timu ambazo hazijapoteza mechi nyumbani sambamba na Yanga, Azam na Mashujaa.
“Hii ni mechi nyingine, tumeshaanza maandalizi dhidi yao, naamini ubora wa kikosi chetu pamoja na ubora wa Kocha Francis Baraza katika mchezo huu tutapambana iwezekanavyo kufanya vizuri,” amesema William.
Ofisa huyo amewataka mashabiki kutoingia uwanjani na matokeo yao akisema: “Matokeo hayapatikani mitandaoni wala nyumbani, yanapatikana uwanjani CCM Kirumba, mashabiki waje kistaarabu kuangalia mechi, kisha warundi nyumbani kwao wakiwa salama.
“Mchezo una matokeo matatu, kufungwa, sare na kushinda, hivyo lazima matokeo kati ya hayo yapatikane baada ya kumalizika dakika 90 za mchezo na yanapaswa kupokelewa vizuri.”