Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, ametoa wito kwa viongozi wa dunia na wale wenye uwezo wa kuanzisha vita kuchagua amani badala ya migogoro, katika ujumbe wake wa kwanza wa Pasaka tangu achaguliwe kuongoza kanisa hilo mwaka jana.
Akizungumza kutoka roshani ya St. Peter’s Basilica mbele ya maelfu ya waumini waliojitokeza katika St. Peter’s Square, Papa Leo XIV alisisitiza umuhimu wa mazungumzo na maridhiano katika dunia iliyogubikwa na vita, chuki na kutojali.
“Wale wote wenye silaha waache kuzitumia. Na wale wenye nguvu ya kuanzisha vita wachague amani. Amani ya kweli haipaswi kulazimishwa kwa nguvu, bali ipatikane kupitia mazungumzo na kuheshimiana,” alisema Papa huyo.

Katika ujumbe wake, Papa Leo XIV alionya kuwa dunia inaelekea kuzoea vurugu na mateso, hali aliyoiita “utandawazi wa kutojali,” akirejea kauli iliyokuwa ikitumiwa na mtangulizi wake, Pope Francis.
Papa huyo pia alitangaza kufanyika kwa ibada maalum ya kuombea amani itakayofanyika Aprili 11 ndani ya St. Peter’s Basilica, akilenga kuhamasisha dunia kusimama pamoja kupinga vita na machafuko.
Katika mahubiri yake ya Pasaka, Papa Leo XIV aligusia changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia ikiwemo vita, mabadiliko ya tabianchi na mateso ya watu wasio na hatia, akisisitiza kuwa ujumbe wa Pasaka unatoa tumaini jipya kupitia Jesus Christ.

Alisema licha ya giza la matatizo yanayoikumba dunia, bado kuna matumaini ya mabadiliko na mwanzo mpya kila siku.
Maelfu ya waumini na watalii walijaa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kushiriki ibada hiyo ya Pasaka, huku wakionesha mshikamano na Papa huyo mpya katika uongozi wake.
Ujumbe wa Papa Leo XIV unakuja wakati dunia ikiendelea kushuhudia migogoro ya kivita katika maeneo mbalimbali, huku akitoa matumaini kuwa viongozi wa dunia watachagua njia ya amani badala ya kuongeza vita.
