Sita zatangulia robo fainali FA Cup Pemba

CHIPUKIZI, Mwenge, Wawi Stars, Azimio, Machomane na Chakechake, zimefuzu robo fainali ya Kombe la FA Kanda ya Pemba, baada ya kufanya vizuri hatua ya 16 bora.

Chipukizi ambayo ilibeba ubingwa huko Pemba msimu uliopita, ilianza kutangulia robo fainali baada ya kuifunga El-gado mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Gombani, mechi iliyochezwa Machi 28, 2026, saa 8:00 mchana.

Mwenge ilifuatia kwa kifunga Bubujiko kwenye Dimba la FFU Finya, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Chakechake iliitoa Small Fighters kwa mikwaju ya penalti 7-6 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Nayo Machomane iliifunga Kambini Heroes mabao 2-0 kwenye Uwanja ya FFU Finya na Wawi Star imefuzu kwa kuitembeza kichapo cha mabao 3-2 timu ya Eleven Boys.

Azimio iliisulubu Afrikan Kivumbi mabao 5-1, mchezo uliochezwa Aprili Mosi, 2026 kwenye Dimba la Mtega, saa 10:00 jioni.

Michuano hiyo, imebakisha viporo vya michezo miwili kukamilisha hesabu kamili za michuano hiyo na Super Falcon itacheza dhidi ya Fufuni wakati Junguni ikikabiliana na New Stone. Mechi hizo zinatarajiwa kuchezwa kati ya Aprili 7 na 8 mwaka huu.

Baada ya kupatikana bingwa wa Kanda ya Pemba, atacheza na bingwa wa Unguja kutafuta bingwa mmoja wa Zanzibar ambaye ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na hivi sasa bingwa mtetezi no KMKM.