Straika Muivory Coast afichua ofa za Yanga, Simba

SIMBA ilikuwa ya kwanza kuiwania saini ya mshambuliaji wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Souleymane Fofana, lakini ghafla watani zao wa jadi, Yanga wakaingilia kati nao wakihitaji huduma ya nyota huyo.

Wakati klabu hizo kongwe zikipambana kuwania saini ya mshambuliaji huyo ambaye yuko kwenye fomu kubwa ya kiwango msimu huu, mwenyewe amefichua tayari amejulishwa juu ya ofa ya Yanga na Simba, huku akisema hana shida ya kujiunga na moja ya timu hizo.

Fofana ameliambia Mwanaspoti kwa simu kuwa, ameshajulishwa na uongozi wake juu ya uwepo wa ofa hizo mbili kutoka Simba na Yanga ambapo ameiachia menejimenti yake kuangalia ni klabu ipi itafikia maslahi yake pamoja na yale ya ASEC Mimosas ambao bado ana mkataba nao.

Mshambuliaji huyo amesema ana taarifa njema juu ya soka la Tanzaia ambapo kwa Yanga kama atamalizana nao atafurahi kujiunga na mastaa wenzake wa nchini kwake Pacome Zouzoua na Yao Kouassi ambao waliitumikia ASEC kwa mafanikio.

“Nimeambiwa kwamba kuna hizo ofa mbili za kutoka Tanzania, kila mchezaji ana ndoto za kutaka kucheza soka sehemu inayopiga hatua lakini mimi bado nina mkataba na ASEC, nimewaachia wasimamizi wangu na uongozi wa klabu uangalie sehemu gani itakuwa muafaka kulingana na maslahi yangu na yale ya klabu,” amesema Fofana.

“Yanga naiona ni timu kubwa na jambo zuri ni kwamba kuna kaka zangu pale Zouzoua (Pacome) na Yao (Kouassi) hawa wote ni wachezaji wenye heshima kubwa, kama unapata nafasi ya kucheza nao pamoja ni jambo la furaha.”

Aidha Fofana akaeleza kuwa Simba pia nayo ni klabu kubwa ambapo alivutiwa na namna aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua alivyoitumikia kwa msimu mmoja tu na kuwa mfungaji bora wa ligi hatua ambayo imempa amani kwamba inawezekana akaja kufanya kazi kwa mafanikio.

“Simba unaona Ahoua (Jean) alipita pale msimu mmoja alikuwa mfungaji bora, hii inakupa picha kwamba kama ukienda sehemu na ukaweka juhudi kila kitu kinawezekana lakini kwasasa ngoja kwanza tuone ni wapi mambo yatakamilika.”

Fofana msimu huu yupo kwenye kiwango bora akifunga mabao 13 kwenye Ligi ya Ivory Coast akiongoza kwa ufungaji lakini pia akiwa na asisti tano na kufanya kuhusika kwenye jumla ya mabao 18 akiwa ndiye staa muhimu kwenye kikosi cha ASEC.

Yanga na Simba zote zinatafuta mshambuliaji wa kati lakini timu yeyote kati ya hizo zikifanikiwa kuinasa saini ya staa huyo itakuwa imelamba dume kwani pia ana ujuzi wa kucheza kama kiungo mshambuliaji akitokea pembeni na katikati.