Tanzania Prisons yagoma kushuka daraja

PAMOJA na Tanzania Prisons kushika nafasi ya pili kutoka mkiani katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 13, nyota wa timu hiyo, bado wana imani ya kusalia msimu ujao wa 2026-2027.

Mwanaspoti lilizungumza na wachezaji wa timu hiyo, baada ya juzi Jumamosi kufungwa mabao 3-0 na Yanga na wamesema katika mechi zilizosalia lolote linaweza likatokea, wakisisitiza hawajakata tamaa, mapambano yanaendelea.

Miongoni mwao ni mshambuliaji George Mpole aliye na mabao manne, ambaye amesema pamoja na changamoto ya kukosa matokeo ya ushindi, hawajaruhusu kukata tamaa badala yake wanaendelea kuzipigia hesabu mechi zilizosalia, huku wakiboresha maeneo yanayohitaji kuongezwa nguvu zaidi.

“Ligi imefikia pagumu sana, lakini hatuna chaguo lingine zaidi ya mapambano na kutupa karata yetu katika mechi zilizopo mbele yetu, bado imani yetu ni kubwa tutasalia katika ligi,” amesema Mpole.

Mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Jeremiah Juma amesema: “Bado tuna nafasi ya kupambana katika mechi zilizopo mbele yetu na ndiyo hamasa tunayopeana wachezaji, tunajua ni ngumu ila tutafanikiwa.”

Mussa Mbisa, kipa wa timu hiyo amesema: “Ingawa mechi za mwishoni zinakuwa ngumu sana kwani kila timu inakuwa na hesabu zake, lakini nina imani tutapambana tuendelee kusalia katika ligi msimu ujao.”

Kocha wa Dodoma Jiji, Aman Josiah aliyewahi kuinusuru Prisons isishuke daraja kwa kucheza mechi za mtoano (playoff) dhidi ya Fountain Gate msimu uliopita, amesema: “Vipindi vigumu katika mpira wa miguu haviwezi kukosekana, mechi bado zipo, lolote linaweza likatokea, hivyo bado Prisons ina nafasi ya kusalia kama ikishinda mechi zilizobaki.”

Tanzania Prisons imesaliwa na mechi 12 kumaliza msimu huu na itacheza dhidi ya KMC (ugenini), TRA United (nyumbani), Mbeya City (nyumbani), Simba (ugenini), Fountain Gate (nyumbani), Azam (ugenini), Pamba Jiji (ugenini), Dodoma Jiji (nyumbani), JKT Tanzania (ugenini), Singida Black Stars (ugenini), Mtibwa Sugar (nyumbani) na Mashujaa (ugenini).