TAUSI FC imemtambulisha Baraka Kilasi kama moja ya makocha watakaounda benchi la ufundi akiungana na makocha wengine Wajerumani wawili ambao ni Paul Gomez na Martin.
Kilasi ambaye ana uzoefu mkubwa katika ukocha amewahi kuwa kocha msaidizi wa Simba SC U20, Tazara FC ya Zambia na Young Boys FC inayoshiriki ligi kuu ya Zambia.
Akizungumza na Mwanaspoti Mkuu wa kitengo cha Habari, Amosi Mlandali amesema bado hawajapata kocha mkuu mwenye vigezo hivyo na hao watatu wapo kwa muda, kwani wanataka kocha mwenye vigezo na wameshapokea CV za makocha wengi ndani na nje.
“Tumeanza bila kocha mkuu, lakini benchi lililopo linaendelea kusaidia timu katika majukumu ya kila siku,” amesema Mlandali na kuongeza Tausi FC haina lengo la kuchukua ubingwa bali kuendeleza vipaji vya wachezaji na kuwauza ligi mbalimbali akimtolea mfano Adama Congo aliyetimkia Dux Lugrono ya Hispania.
“Tuna malengo ya kuendeleza wachezaji wetu, kila mchezaji anatamani kucheza nje ya nchi, hivyo tunahitaji makocha watakaowakuza na kuwafikisha huko.”
Ameongeza mbali na hilo, klabu hiyo pia inalenga kuzalisha wachezaji watakaoitumikia timu ya taifa.
