Global Publishers
April 6, 2026
0 Comments
Aliyekuwa mbunge wa Marekani, Marjorie Taylor Greene, amemkosoa vikali Rais Donald Trump baada ya kutoa kauli kali dhidi ya Iran siku ya Pasaka.
Trump aliandika kupitia mtandao wake wa Truth Social akitishia mashambulizi makubwa dhidi ya Iran, akisema kuwa nchi hiyo ina saa 48 kufungua njia ya meli katika Strait of Hormuz, vinginevyo “jahannamu itashuka juu yao.”
Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa, huku Greene akimuita Trump amechanganyikiwa na hata kudai kuwa si Mkristo. Kupitia mtandao wa X, Greene alisema viongozi wote wanaojiita Wakristo ndani ya utawala wa Trump wanapaswa kutubu na kumzuia rais huyo.
Greene pia alilaumu Marekani na Israel kwa kuanzisha vita dhidi ya Iran, akisema hatua hiyo imechangia kufungwa kwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani. Njia hiyo hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta ya dunia, hivyo hali hiyo imeongeza bei za nishati kimataifa.

Aidha, alisisitiza kuwa Israel tayari ina silaha za nyuklia na ina uwezo wa kujilinda bila msaada wa Marekani, huku akionya kuwa vita hiyo inaathiri raia wasio na hatia.
Mgogoro kati ya Greene na Trump umeendelea tangu mwaka jana, hasa baada ya kutofautiana juu ya mashambulizi dhidi ya Iran na masuala mengine ya kisiasa. Hatimaye, Trump aliondoa uungwaji mkono wake kwa Greene, jambo lililosababisha aondoke rasmi katika siasa za bunge mapema mwaka huu.
Katika ujumbe wake wa mwisho, Greene aliwakumbusha Wakristo kuwa mafundisho ya Jesus Christ yanasisitiza upendo na msamaha, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kutafuta amani badala ya kuongeza vita.