Rais wa Marekani Donald Trump ameibua taharuki mpya kimataifa baada ya kutoa kauli kali dhidi ya Iran kupitia ujumbe mkali aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, akisisitiza kuwa nchi hiyo ifungue mara moja Mlango wa Hormuz au ikabiliwe na mashambulizi makubwa ya kijeshi.
Katika ujumbe huo uliosheheni lugha kali, Trump alionya kuwa iwapo Iran haitafungua njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta, itakumbana na madhara makubwa, akidai kuwa hatua zitakazochukuliwa zitakuwa za kipekee na zenye athari kubwa kwa miundombinu ya nchi hiyo.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi huyo kuipa Iran muda wa saa 48 kufungua Mlango wa Hormuz, huku akisisitiza kuwa “muda unaisha” na maamuzi magumu yanakaribia kuchukuliwa. Trump pia alidokeza uwezekano wa kushambulia mitambo ya umeme na madaraja muhimu nchini Iran ikiwa masharti hayo hayatatimizwa.
Aidha, Trump alieleza kuwa Marekani iko tayari kuchukua hatua zaidi ikiwa Iran haitafikia makubaliano ya haraka, ikiwemo kudhibiti rasilimali zake za mafuta. Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano, akidai kuwa mazungumzo yanaendelea na yanaweza kuzaa matokeo chanya.
Kwa upande mwingine, Iran imejibu kwa msimamo mkali, ikionya kuwa itaigeuza eneo lote la Mashariki ya Kati kuwa hatari kwa wanajeshi wa Marekani iwapo vita vitaongezeka. Msemaji wa serikali hiyo alisisitiza kuwa jaribio lolote la kuishinda Iran litageuka kuwa changamoto kubwa kwa wapinzani wake.
Mvutano huu umechangiwa zaidi na hatua za kijeshi zilizochukuliwa na pande zote, ikiwa ni pamoja na taarifa za kuwekwa kwa mabomu ya majini na mashambulizi dhidi ya meli za mafuta katika Mlango wa Hormuz, eneo ambalo linapitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote duniani.
Wakati huo huo, Trump alitangaza mafanikio ya operesheni ya kijeshi ya kuwaokoa marubani wa Marekani waliokuwa wametekwa baada ya ndege yao kudunguliwa ndani ya anga ya Iran. Operesheni hiyo, iliyofanywa na vikosi maalum, imeelezwa kuwa moja ya operesheni hatari na ya kipekee katika historia ya kijeshi ya Marekani.
Hali inaendelea kuwa tete huku dunia ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya mgogoro huo, ambao unaweza kuwa na athari kubwa kiuchumi na kisiasa endapo hautapatiwa suluhisho la kidiplomasia kwa wakati.