Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amewataka wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu nchini na vijana kuendelea kulinda na kutetea misingi ya Muungano iliyoachwa na Waasisi.
Mhe. Mhandisi Masauni ameyasema hayo Aprili 06, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano maalum la kumuenzi aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Waziri Masauni amesema mwasisi huyo wa Muungano ameacha alama na historia ya kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo, juhudi zilizotokana na mchango alioutoa katika kuwaunganisha Watanzania na kupambania maslahi ya wananchi wanyonge.
“Leo hii tunapomuenzi Sheikh Abeid Amani Karume tuna mengi ya kujifunza kutoka kwake kwani tumejionea jinsi alivyojali na kutetea maslahi ya wananchi wanyonge na zaidi ni juhudi zake katika kuasisi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964” amesema Mhandisi Masauni.
Aidha Mhe. Masauni amemtaja Sheikh Abeid Amani Karume Zanzibar kuwa ni kiongozi imara aliyesimamia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Zanzibar juhudi ambazo zimendelea kusimamiwa katika awamu mbalimbali za uongozi.
Amesema Sheikh Abeid Amani Karume ataendelea kukumbukwa na Watanzania kutokana na kuibua sera zilizogusa hisia za wananchi walio wengi ikiwemo ugawaji bure wa ardhi, utoaji wa elimu bure, matibabu ya bure na ujenzi wa makazi ya kisasa.
“Sheikh Karume aliishi ndoto ya muda mrefu ya uanamajumui wa kiafrika katika kuunganisha Bara zima la Afrika na kuunda Shirikisho la Afrika kwa vitendo na alifanya mambo mengi muhimu ambayo kamwe hayawezi kusahaulika” amesema Mhe. Mhandisi Masauni.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi amesema kongamano hilo ni la kwanza kufanyika kwa upande wa Tanzania Bara ambalo linalenga kuhamasisha vijana kutambua mchango wa waasisi wa muungano ikiwemo Sheikh Abeid Amani Karume.
Amesema katika kuchagiza elimu ya Muungano, Ofisi hiyo imeandaa programu ya elimu kwa umma ambayo imekusudia kuelimisha wananchi wa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo vijana na wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu nchini.
Kongamano hilo la siku moja limeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa kushirikiana na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza wakati akifungua Kongamano la kumbukizi ya miaka 54 ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Aprili 6, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza wakati akifungua Kongamano la kumbukizi ya miaka 54 ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Aprili 6, 2026.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la kumbukizi ya miaka 54 ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Aprili 6, 2026.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la kumbukizi ya miaka 54 ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Aprili 6, 2026.
Baadhi ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu waliohudhuria Kongamano la kumbukiziya miaka 54 ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani katika Ukumbi wa Karimjee jijiniDar es Salaam, Aprili 6, 2026.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)