WAZIRI MKUU AKAGUA MADHARA YA MOTO SOKO LA SIMU 2000, AAGIZA HATUA ZA HARAKA KUREJESHA BIASHARA

-Asema Serikali itatoa kauli baada ya uchunguzi

-Aagiza vibanda vipya vigawiwe kwa wafanyabiashara halisi

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza hatua za haraka kurejesha shughuli za biashara kufuatia ajali ya moto ulioteketeza Soko la Mawasiliano (Simu 2000) lililopo katika Kata ya Sinza, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Ameyasema hayo Aprili 6, 2026, alipofika kukagua madhara ya tukio hilo la moto lililotokea Aprili 4, 2026, ambapo takribani vibanda 500 vya wafanyabiashara wadogo viliteketea.

Akizungumza na wafanyabiashara hao, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu tukio hilo na itatoa kauli rasmi baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kina ulioelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mheshimiwa Rais amepata taarifa ya jambo hili, anawapa pole sana na ameelekeza uchunguzi wa kina ufanyike ili tujue chanzo cha tatizo hili. Na kazi hiyo imekwisha kuanza ili tuweze kupata undani wa chanzo cha jambo hili lililojitokeza,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu ameagiza eneo la soko hilo kusafishwa mara moja ili kuruhusu wafanyabiashara kuanza taratibu za kurejesha shughuli zao.

“Mkurugenzi, ukitoka hapa leo wakati unamalizia siku… kesho hapa pote pasafishwe. Hii kazi ya kusafisha kesho iishe,” amesema.

Amesema Serikali itashirikiana na taasisi za kifedha kusaidia wafanyabiashara wenye mikopo waliopoteza mitaji yao, pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaongezea muda wa kurejesha mikopo hiyo na kuwezesha upatikanaji wa mikopo mipya yenye nafuu kupitia mamlaka za serikali za mitaa.

“Mkurugenzi sasa kwenye mikopo mipya nenda kaangalie una ukoko gani… tufanye kipaumbele kwa hawa ambao mtaji wao umeungua ili wapate haraka,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kuwepo kwa eneo la stendi katika mpango wa ujenzi wa soko hilo ili kurahisisha shughuli za biashara.

Kadhalika, amekemea vitendo vya ulanguzi wa vibanda katika masoko na kusisitiza kuwa vibanda vitolewe kwa wafanyabiashara halisi wanaofanya biashara.

Vilevile, amewataka wananchi kushirikiana katika kulinda amani na utulivu wa nchi, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa shughuli zote za kiuchumi. “Ni lazima tuwe na amani kwenye nchi yetu. Kila Mtanzania awe mdau wa amani katika nchi yetu,” amesema.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuheshimu sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi, akieleza kuwa ndiyo mhimili mkuu wa ajira kwa Watanzani