Waziri Mkuu aonya watumishi wanaojimilikisha vizimba vya biashara

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewaonya watumishi wa Serikali wenye tabia ya kuchukua vizimba vya biashara katika masoko bila kuvifanyia shughuli yoyote, akisema tabia hiyo ni ya ulanguzi na inawaumiza wafanyabiashara halali wanaotegemea maeneo hayo kujipatia kipato.

Amesema suala hilo halitavumiliwa na Serikali huku akitaka usimamizi thabiti wakati ugawaji wa vizimba unapofanywa katika soko lolote ili kuhakikisha wanaopewa ni wanaomiliki biashara.

Baadhi ya watendaji kujimilikisha vizimba kisha kukodisha watu wengi kwa maeneo yenye yaliyochangamka au kubaki wazi ni suala linalopigiwa kelele kwa muda mrefu. Suala hilo husababisha wachuuzi wadogo kukosa maeneo ya kufanyia biashara ilihali watendaji hao wakiwa wameyahodhi bila kuyatumia au kukodisha kwa bei ya juu.

Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Simu2000 ambao waliunguliwa na biashara zao katika moto uliotokea Aprili 4 mwaka huu na kusababisha hasara.

Amesema baadhi ya watu wamegeuza fursa za biashara kuwa njia ya kujinufaisha bila kufanya kazi jambo ambalo ni kinyume na taratibu na linawaumiza wengine.

Baadhi ya wafanyabiashara waliojitokeza kumsikiliza Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba alipofika kukagua madhara ya tukio hilo la moto lililotokea Aprili 4, 2026 katika Soko la Mawasiliano (Simu 2000) lililopo katika Kata ya Sinza, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.    

“Wapo wanaochukua maeneo hawafanyi biashara, wanakaa kama walanguzi, wanaweka chazo cha ziada, wanakodisha kwa wengine na kuongeza gharama kwa wafanyabiashara wadogo. Hii haikubaliki hata kidogo,” amesema.

Amesema ndani yao wapo hata watumishi wa Serikali wanaojihusisha na vitendo hivyo: “Kama wewe uko serikalini umeshapata fursa na unalipwa kwa kodi za hawa wafanyabiashara, ridhika na hicho. Kama unataka kufanya biashara, fanya halali siyo hii ya kupandisha gharama bila kufanya kazi.”

Dk Mwigulu aliziagiza mamlaka za mikoa na wilaya kuhakikisha ugawaji wa vizimba katika maeneo yote yanayojengwa kuhakikisha unazingatia haki na unawalenga watu wanaofanya biashara moja kwa moja, huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaoendesha ulanguzi huo.

“Kama kuna mtu anajaribu kukwepa utaratibu huu, ajaribu lakini ajue si kila kiberiti kitawaka, vingine vitamchoma,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa maagizo ya haraka ya kusafishwa kwa eneo hilo ili shughuli za biashara zianze kwa hatua ndogondogo wakati uchunguzi ukiendelea.

“Mkurugenzi, hakikisha kesho eneo hili linasafishwa kabisa ili wale wanaoweza kuanza biashara ndogondogo waanze mara moja maisha yaendelee,” ameelekeza.

Amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan amepokea taarifa ya tukio hilo, ametuma salamu za pole kwa waathirika na kuagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

“Tutasubiri taarifa ya uchunguzi ndipo tutoe maelekezo ya kina zaidi,” amesema.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali imepokea hoja zote kutoka kwa viongozi wa eneo hilo wakiwemo mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na mbunge, na baadhi ya maamuzi yatafanywa baada ya kupatikana kwa undani wa tukio.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kupanga miundombinu ya masoko kwa kuzingatia mahitaji yote muhimu, akieleza kuwa mara nyingi maeneo ya biashara hujengwa bila kuzingatia huduma muhimu kama vituo vya magari.

Baadhi ya mabaki ya vibanda vya wafanyabiashara yakionekana kufuatia ajali ya moto ulioteketeza Soko la Mawasiliano (Simu 2000) lililopo katika Kata ya Sinza, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

“Biashara inaendana na stendi. Huwezi kujenga soko bila kufikiria magari yatakaposimama. Tukikosea hapo, baada ya muda tunabomoa tena ili kurekebisha hii siyo sahihi,” amefafanua.

Kwa upande wa wafanyabiashara waliopata hasara au waliokuwa na mikopo, Waziri Mkuu ameagiza uongozi wa mkoa na wilaya kukusanya taarifa zao na kushirikiana na taasisi za kifedha ili kupata suluhisho la haraka.

“Pateni orodha ya wote walioathirika, mjue wamekopa wapi, tuzungumze na taasisi husika ili wapate nafuu na waweze kuendelea na biashara zao,” amesema.

Katika kupunguza makali ya hasara, Dk Nchemba ameelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo, kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya uwezeshaji zinatolewa kwa wafanyabiashara hao ili kuwasaidia kurejea kwenye shughuli zao bila kuchelewa.

Amesisitiza kuwa hakuna sababu ya ucheleweshaji wakati tayari kuna wafanyabiashara walioathirika na wanaohitaji mtaji wa kuanza upya.

“Fedha hizi zipo kwa ajili ya wananchi, si za kukaa kwenye akaunti. Toeni kwa haraka kwa wale waliostahili ili waweze kurejea kwenye biashara zao,” amesema.

Amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri kupitia mifumo ya mikopo na kuhakikisha wale waliopata hasara wanapewa kipaumbele katika mgawo huo.

 “Wale ambao tuna uhakika wameathirika, wapeni kipaumbele. Hii siyo fedha ya kusubiri taratibu ndefu ni ya kuwainua wananchi haraka,” amesema.