Waziri Mkuu atangaza ahueni kwa waathirika wa moto Simu2000

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameagiza uongozi wa mkoa na wilaya kukusanya taarifa za wafanyabiashara waliopata hasara au waliokuwa na mikopo kutokana na moto uliounguza biashara zao kwenye soko la Simu2000.

Amesema taarifa hizo ni kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara hao kushirikiana na taasisi za kifedha ili kupata suluhisho la haraka la mikopo yao.

 “Pateni orodha ya wote walioathirika, mjue wamekopa wapi, tuzungumze na taasisi husika ili wapate nafuu na waweze kuendelea na biashara zao,” amesema.

Kauli hiyo ameitoa leo Aprili 6,2026 alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Simu2000, waliokumbwa na hasara kufuatia ajali ya moto uliotokea Aprili 4 mwaka huu na kuteketeza mali zao.

Pia, Dk Mwigulu amezielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo, kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili uwezeshaji zinatolewa kwa wafanyabiashara hao ili kuwasaidia kurejea kwenye shughuli zao bila kuchelewa.

Amesisitiza kuwa hakuna sababu ya ucheleweshaji wakati tayari kuna wafanyabiashara walioathirika na wanaohitaji mtaji wa kuanza upya.

“Fedha hizi zipo kwa ajili ya wananchi, si za kukaa kwenye akaunti. Toeni kwa haraka kwa wale waliostahili ili waweze kurejea kwenye biashara zao,” amesema.

Amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri kupitia mifumo ya mikopo na kuhakikisha wale waliopata hasara wanapewa kipaumbele katika mgao huo.

 “Wale ambao tuna uhakika wameathirika, wapeni kipaumbele. Hii siyo fedha ya kusubiri taratibu ndefu ni fedha ya kuwainua wananchi haraka,” amesema.

Pia, amewaonya watumishi wa Serikali wanaojihusisha na tabia ya kuchukua vizimba vya biashara katika masoko bila kuviendeleza kibiashara, akisema hatua hiyo ni ulanguzi unaowaumiza wafanyabiashara halali wanaotegemea maeneo hayo kujipatia kipato.

Amesema Serikali haitavumilia vitendo hivyo, na kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa usimamizi madhubuti katika mchakato wa ugawaji wa vizimba ili kuhakikisha vinatolewa kwa watu wanaojishughulisha moja kwa moja na biashara.

Dk Mwiguli amesema baadhi ya watu wamekuwa wakigeuza fursa za biashara kuwa njia ya kujinufaisha binafsi bila kushiriki katika shughuli halisi za kiuchumi, hali ambayo ni kinyume cha taratibu na inawakosesha wengine haki ya kupata maeneo ya kufanyia biashara.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za kudhibiti vitendo hivyo ili kulinda masilahi ya wafanyabiashara na kuhakikisha fursa zilizopo zinawanufaisha walengwa stahiki.

 “Wapo wanaochukua maeneo hawafanyi biashara, wanakaa kama walanguzi, wanaweka chazo cha ziada, wanakodisha kwa wengine na kuongeza gharama kwa wafanyabiashara wadogo. Hii haikubaliki hata kidogo,” amesema.

Amesema ndani yao wapo hata watumishi wa Serikali wanaojihusisha na vitendo hivyo, “Kama wewe uko serikalini umeshapata fursa na unalipwa kwa kodi za hawa wafanyabiashara, ridhika na hicho. Kama unataka kufanya biashara, fanya halali siyo hii ya kupandisha gharama bila kufanya kazi.”

Mwigulu ameziagiza mamlaka za mikoa na wilaya kuhakikisha ugawaji wa vizimba katika maeneo yote yanayojengwa unazingatia haki na unawalenga watu wanaofanya biashara moja kwa moja, huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaoendesha ulanguzi huo.

“Kama kuna mtu anajaribu kukwepa utaratibu huu, ajaribu lakini ajue si kila kiberiti kitawaka, vingine vitamchoma,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa maagizo ya haraka ya kusafishwa kwa eneo hilo ili shughuli za biashara ziweze kuanza tena kwa hatua ndogondogo wakati uchunguzi ukiendelea.

“Mkurugenzi, hakikisha kesho eneo hili linasafishwa kabisa ili wale wanaoweza kuanza biashara ndogondogo waanze mara moja maisha yaendelee,” ameelekeza.

Amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan amepokea taarifa ya tukio hilo, ametuma salamu za pole kwa waathirika na kuagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha ajali hiyo. “Tutasubiri taarifa ya uchunguzi ndipo tutoe maelekezo ya kina zaidi,” amesema.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali imepokea hoja zote kutoka kwa viongozi wa eneo hilo wakiwemo mkuu wa mkoa, wilaya na mbunge, na baadhi ya maamuzi yatafanywa baada ya kupatikana kwa undani wa tukio hilo.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kupanga miundombinu ya masoko kwa kuzingatia mahitaji yote muhimu, akieleza kuwa mara nyingi maeneo ya biashara hujengwa bila kuzingatia huduma muhimu kama vituo vya magari.

“Biashara inaendana na stendi. Huwezi kujenga soko bila kufikiria magari yatakaposimama. Tukikosea hapo, baada ya muda tunabomoa tena ili kurekebisha hii siyo sahihi,” amefafanua.

Awali, akizungumzia ugawaji wa maeneo ya biashara, Samadou Bakari mfanyabiashara wa soko hilo ameomba kamati iliyokuwa imechaguliwa kwa ajili ya maboresho na uongozi wa soko hilo itenguliwe badala yake wachaguliwe wengine kwa ajili ya kuwawakilisha wafanyabiashara hao.

 Moto ukiteketeza mabanda Aprili 4, 2026 katika soko la Simu 2000 lililopo katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Amesema uongozi wa Mwenyekiti wa soko hilo Mussa Ndile wamekuwa wakigawa maeneo na baadhi wanajigawia wenyewe.

“Hatutaki mtu anayechukua fursa kwa kuwaumiza watu, hili ni jambo linatokea, Waziri Mkuu tusingeongelea hili suala ukasema wasafishe hapa ungekuja kesho hapa ungeambiwa hili eneo la mtu fulani amepangishwa, hili eneo ni la mtu fulani limepangishwa,” amesema.

Akijibu suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema awali eneo hilo lilikuwa na siasa ambapo watu walifanya siasa kwa migongo ya wafanyabiashara na kujipatia masilahi yao.

“Niliwaeleza jambo hili kuwa hatutalifumbia macho na nitalisimamia wenyewe, nitataka kujua nani anaingia ametoka wapi na amefikaje hapa, hii kamati nilisema hatuundi mbingu mpya, hatutaki kumuonea mtu, wafanyabiashara wakisema hatutaki hatutaki, wakisema tunataka tunataka,” amesema.

Amesema kamati ya usalama wa wilaya itakaa eneo hilo kuhakikisha kuwa wanaochaguliwa wanakuwa ni wale wanaohitajika na wananchi sambamba na kuimarisha ulinzi wa mali zao.

Mfanyabiashara mwingine, Tusamo Kibule ameomba suala la uwepo wa stendi katika eneo hilo kupewa kipaumbele ili kutengeneza mzunguko wa watu wanaoweza kusisimua biashara.

Amesema kuna ramani ambayo wafanyabiashara waliona inafaa na waliambiwa waichore na kupelekwa halmashauri, lakini iliyorudi ni waliyokuwa wametengeneza wao ambayo ina mapungufu mengi.

“Suala la uwepo wa stendi lilikuwa limezingatiwa katika ramani ambayo tulikuwa tumechorwa, kwa sababu uko hapa tunaamini matatizo yametokea lakini inaweza kuwa chanzo cha kuondoa matatizo mengi zaidi, tunaomba ramani iliyokuwa imechorwa muangalie umuhimu wake na namna inavyoweza kutumika kwa ajili ya faida ya wote.”

“Kuweka miundombinu ambayo inaweza kuwa faida kwa wafanyabiashara na soko ambalo linaloweza kuwafanya halmashauri kupata ushuru kwa urahisi, tuogope kujenga eneo ambalo mfanyabiashara hafanyi biashara na halmashauri haipati mapato, kama sijauza uwezekano wa kulipa mapato nakuwa sina,” amesema.

Katika hatua nyingine mfanyabiashara huyo ametaka njia ya haraka iangaliwe ili kuwasaidia kurudi katika shughuli zao ikiwemo kuwapatia mikopo isiyokuwa na masharti mengi.

Suala la uwepo wa stendi liligongelewa msumari na Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo ambaye amesema ili soko lifanye kazi kwa ufanisi ni lazima kuwe na wateja ambao hawawezi kupatikana bila kituo cha mabasi.

“Changamoto huleta fursa, changamoto hii tunashukuru umekuja kutufariji lakini ni fursa pia kwani uwepo wako hapa kuna changamoto tunaomba ziishe ikiwemo stendi,” amesema Mkumbo.

Amesema awali wafanyabiashara hao awali walipaswa kuondoka lakini walisimama kidete kuhakikisha wanaendelea kubaki eneo hilo.