Zijue faida za safari ya wanaanga wa NASA mwezini

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku sita tangu Shirika la Anga la Marekani (NASA) kuzindua rasmi safari yake ya mwezini kupitia chombo cha Artemis II, imeelezwa kuwa tafiti zinazofanyika angani zina matokeo ya moja kwa moja kwa jamii, hususan katika sekta za afya, mawasiliano na uchumi.

Miongoni mwa tafiti zinazoenda kufanyika ni pamoja na utafiti wa seli tiba (stem cells), unaolenga kutafuta tiba ya magonjwa sugu kama saratani na magonjwa ya damu.

Aprili mosi, 2026, NASA iliwapeleka wanaanga wanne katika safari ya kuzunguka mwezi, hatua kubwa mbele katika uchunguzi wa anga za mbali.

Safari hiyo inayoongozwa na wanaanga hao, akiwemo mwanamke mmoja, Christina Koch, wamo Reid Wiseman, Victor Glover na Jeremy Hansen, si tukio la kawaida, kwani linarudiwa kwa mara nyingine baada ya miaka 50.

Ni mchakato mrefu unaohusisha mafunzo makali, maandalizi ya kisayansi na teknolojia ya hali ya juu. Wanaanga huchaguliwa kwa vigezo vigumu, ikiwemo afya bora, taaluma za sayansi na uhandisi, pamoja na uwezo wa kufanya kazi katika mazingira hatarishi.

Swali kubwa ambalo wengi wanajiuliza, wanaanga hawa wanakwenda kufanya nini mwezini? Kama hukuwahi kujua, safari hii ina manufaa makubwa kwa kila binadamu anayeishi katika sayari ya dunia.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, misheni ya Artemis II itaweka msingi kwa wanaanga kuchunguza mwezi kwa ajili ya ugunduzi wa kisayansi, manufaa ya kiuchumi, na kusaidia kujenga msingi kwa safari za kwanza za wanaanga kuelekea sayari ya Mars.

Safari za anga zinazoendeshwa na NASA, kwa kushirikiana na kampuni binafsi kama SpaceX na Northrop Grumman, zimeendelea kuonesha mchango mkubwa katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na maisha ya binadamu duniani.

Licha ya kuonekana kama shughuli za mbali na maisha ya kila siku, wataalamu wanasema tafiti zinazofanyika angani zina matokeo ya moja kwa moja kwa jamii, hususan katika sekta za afya, mawasiliano na uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa za kisayansi, tafiti zinazofanyika katika International Space Station (ISS) zimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya duniani.

Miongoni mwa tafiti hizo ni pamoja na utafiti wa seli tiba (stem cells), unaolenga kutafuta tiba ya magonjwa sugu kama saratani na magonjwa ya damu.

Pia, utafiti wa mfumo wa bakteria tumboni (gut microbiome) unatarajiwa kusaidia kuboresha kinga ya mwili na lishe ya binadamu.