Arusha. Nchi za Afrika zimetakiwa kuongeza uwekezaji katika kujenga jamii zinazozingatia haki, huruma na utu wa binadamu kwa mustakabali wa amani za nchi zao dhidi ya matukio ya umwagaji damu.
Wito huo umetolewa leo Aprili 7, 2026 jijini Arusha na meya wa jiji hilo, Maximilian Iranghe katika maadhimisho ya miaka 32 tangu kutokea mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994 nchini Rwanda, maarufu kama Kwibuka 32.
Iranghe amesema mauaji ya kimbari ni ukumbusho wa athari mbaya za chuki, mgawanyiko na kudhalilishwa kwa utu wa binadamu vinapoachwa bila kudhibitiwa.
“Ni wajibu wetu kama mataifa, taasisi na watu binafsi kukataa aina zote za ubaguzi, kutovumiliana na uchochezi wa vurugu, pia, ni lazima tuzungumze wazi dhidi ya dhuluma, hata pale inapokuwa si rahisi ili kuzuia mbegu za migogoro zisikue na kuwa vurugu,” amesema.
Amesema amani haiwezi kupatikana kwa bahati mbaya, bali inahitaji uwekezaji wa makusudi katika jamii zinazojali haki, huruma na utu wa binadamu.
Maadhimisho hayo yaliyobeba kaulimbiu “Kumbuka, Ungana, Jenga Upya” inaadhimishwa kila mwaka kuwakumbuka waathirika milioni moja, wengi wao wakiwa Watutsi pamoja na Wahutu wenye msimamo waliouawa ndani ya siku 100 pekee mwaka 1994.
Tukio hilo lilianza kwa maandamano ya kutoka Makao Makuu ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) waliotembea katika barabara ya Makongoro, wakipitia makutano ya Mwenge hadi Pangani na baadaye barabara ya Uhuru (Sokoine), kabla ya kuelekea Mnara wa Saa unaotambulika kama kitovu cha Afrika.
Baadaye, washiriki walirejea katika jengo la EAC ambako mashada ya maua yaliwekwa katika mnara maalumu kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa mauaji hayo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanyarwanda katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, Flavia Busingye amesema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kikanda la tafakari na mshikamano.
“Tumekusanyika hapa si kwa ajili ya kukumbuka tu, bali pia kuthibitisha upya dhamira yetu ya pamoja ya kusimamia ukweli na kuhakikisha maovu kama haya hayajirudii tena,” amesema.
Busingye amesisitiza umuhimu wa kuwafundisha vijana ili waelewe historia hiyo. Amesema uwepo wa simulizi kinzani baadhi zikiwa za ukweli na nyingine za upotoshaji unaleta changamoto kubwa hasa kwa vijana wanaotafuta uelewa sahihi.
“Tunapaswa kulinda ukweli, umoja na mustakabali wetu kwa kukataa upotoshaji na kuhakikisha historia haibadilishwi, iwe ni majumbani, katika jamii au katika taasisi,” amesema.
Pia, ametoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki na wadau mbalimbali kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya kutowajibika na kuhakikisha haki inatendeka bila upendeleo.
Kwa upande wake, Dorcas Omukhulu, akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia miundombinu, sekta za uzalishaji na siasa, Andrea Aguer Malueth amesema mauaji hayo hayakuwa tatizo la Rwanda pekee bali janga lililogusa ukanda mzima na dunia kwa ujumla.
Amesema mauaji hayo hayakutokea ghafla, bali yalitanguliwa na dalili wazi kama hotuba za chuki, ubaguzi wa kimfumo na mipango ya vurugu.
“Licha ya onyo kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu na waangalizi wa kimataifa, dunia ilishindwa kuchukua hatua kwa wakati,” amesema.
Amesema baadhi ya dalili hizo bado zinaonekana katika baadhi ya maeneo ya ukanda huu, ikiwemo lugha ya kichochezi, siasa za ubaguzi na udhaifu wa taasisi za kusimamia haki.
Naye msaidizi maalumu wa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Diallo Nouhou Madan amesema mauaji ya kimbari ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaopaswa kupingwa kwa nguvu zote.
“Sisi tuliopo leo tunabeba jukumu la kuhakikisha kuwa kauli ya ‘isitokee tena’ haibaki maneno tu, bali inatekelezwa kwa vitendo kupitia ushirikiano, mawasiliano na hatua madhubuti,” amesema.
Ameongeza kuwa migogoro mingi duniani inachochewa na dhuluma na ukosefu wa haki huku akisisitiza kuwa maisha ya binadamu ni ya thamani isiyopaswa kupuuzwa.
