Baada ya sare na Azam, mabosi Simba wajifungia na mastaa, wasisitiza jambo

BAADA ya mchezo dhidi ya Azam uliomalizika kwa matokeo ya 0-0, mashabiki wa Simba walikuwa nje wakilia na uamuzi wa waamuzi waliochezesha, lakini mabosi wao wakajifungia kwa dakika 35 wakiteta na mastaa wote wa kikosi hicho huku jambo moja likisisitizwa.

Simba ilitoa sare ya tano msimu huu ikilingana na vinara wa ligi Yanga na TRA United inayokwenda kukutana nayo Aprili 9 mwaka huu Arusha .

Baada ya mchezo huo uliochezwa Aprili 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar, bosi mmoja tu wa Simba Sued Mkwabi ndiye aliyeondoka haraka uwanjani hapo kwa dharura zake binafsi lakini wengine wote wakaingia vyumbani kisha mlango kufungwa wakiteta na wachezaji wao.

Kwenye kikao hicho, Mwanaspoti limepenyezewa vigogo hao waliwapa pole na kuwapongeza wachezaji wao namna walivyopambana kutafuta ushindi lakini bahati haikuwa upande wao na kuwataka wasikate tamaa.

Hata hivyo, wakati mabosi hao wakisisitiza mapambano yaendelee, wenyewe wakasisitizana wanahitaji kutafuta washambuliaji wawili wa maana kwa msimu ujao kwani kikosi chao bado kinahitaji wenye ubora zaidi.

Simba hadi sasa dua zao zipo kwa mshambuliaji wao Seleman Mwalimu ambaye ndiye anayeongoza kwa ufungaji akiwa na mabao sita, pia  kwenye michezo mitatu ya dabi hakufunga bao lolote likakubaliwa.

“Tulikuwa tunawafariji wachezaji wetu, tulicheza vizuri sana tuliikamata mechi kwenye muda mwingi lakini hata nyie mmeona namna tulivyoshindwa kuzitumia nafasi, na zingine waamuzi wakashindwa kuamua vizuri,” amesema bosi huyo wa Bodi wa Wakurugenzi ndani ya Simba.

“Zile mbili zilikuwa penalti lakini Simba tumeendelea kunyongwa na maamuzi kama haya, ukiondoa hilo tumekubaliana tunatakiwa kuendelea kutafuta washambuliaji, hatutakiwi kuwa na nguvu kama hii ambayo tunayo msimu huu kule mbele.

“Mwalimu (Seleman) anafanya vizuri lakini anahitaji watu wa kumsaidia ili timu ipate kikubwa zaidi na hata makocha wanasisitiza hilo, kwa hiyo tutaendelea kupambana, tumewaambia wachezaji ile ya Azam imekwisha turudishe akili zetu tunapowafuata TRA United kwani nayo ni mechi ngumu.

“Tuliwafunga nyumbani (TRA United) lakini haitakuwa rahisi kukubali kufungwa mara mbili, wana timu nzuri, kwahiyo hatutaki wachezaji waingie kwenye mchezo huo wakiwa wamenyong’onyea kwa sare hii ya Azam, ligi bado iko wazi na ni ngumu.”

Aprili 9 mwaka huu, Simba itakuwa Arusha kucheza dhidi ya TRA United, baada ya mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kuchezwa Machi 14 mwaka huu kuahirishwa siku ya mchezo kufuatia mvua kubwa kunyesha na kusababisha maji kujaa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, hivyo kufanya mpira kushindwa kutembea uwanjani.