Dar/Dodoma. Sakata la kupanda kwa bei ya mafuta nchini limekiibua Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichoielekeza Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku na kuhamasisha kupunguzwa matumizi ya nishati hiyo katika ofisi za umma.
Kupanda kwa bei ya nishati hiyo kumetokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, vikiihusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran, na kuathiri mitambo na miundombinu ya uzalishaji na usafirishaji wa nishati hiyo.
Kutokana na vita hivyo, Iran imeufunga mlango wa Hormuz unaopitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa kwenda mataifa mbalimbali duniani, ikisema itaufungua iwapo Marekani italipia fidia za uharibifu iliyousababisha kwa mashambulizi yake.
CCM imekuja na maelekezo hayo kwa Serikali, ikiwa ni siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoa mapendekezo manne kwa Serikali ili kuleta unafuu wa gharama za nishati hiyo.
Chadema kimependekeza Serikali kuweka ruzuku kwenye mafuta, kutangaza mpango wa dharura wa upatikanaji wa huduma hiyo, kuwepo kwa utaratibu wa uagizaji wake na kudhibiti bei ili wananchi wawe na unafuu.
Maelekezo ya Chadema yalitolewa na Makamu Mwenyekiti wake (Bara), John Heche, alipozungumza kupitia mitandao ya kijamii. Alipendekeza kuwa ili wananchi wawe na unafuu katika huduma ya mafuta, ni lazima Serikali iondoe tozo zote kwenye lita moja ya mafuta.
“Jambo hilo liendane na uwekaji wa utaratibu wa uagizaji wa bei ya mafuta katika hali iliyopo sasa nchini. Jambo la pili, mamlaka itangaze mpango wa ahueni kwa wananchi kwa muda wa siku 60 hadi 90 kwa kutoa ruzuku ili kuwalinda wananchi, hasa katika usafirishaji na kilimo,” alisema Heche.
Leo, Jumanne Aprili 7, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, amesema chama hicho kinaielekeza Wizara ya Nishati kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku katika nishati.
“Chama kinaielekeza wizara kuangalia namna ya kutoa ruzuku, kama ambavyo Rais alifanya mwaka 2022 alipotoa zaidi ya Sh100 bilioni kuleta unafuu kwa wananchi wetu waendelee kufurahia matunda ya nchi yao,” amesema.
Agizo lingine la chama hicho, kwa mujibu wa Kihongosi, ni Serikali ihamasishe kupunguza matumizi ya nishati ya mafuta katika ofisi zake, binafsi na za umma, ili changamoto zinapotokea kuwepo uwezo wa kujiendesha kwa njia za nishati mbadala, ikiwemo gesi asilia.
Pia amesema chama hicho kinaitaka Serikali kuhakikisha mafuta yanapatikana pamoja na changamoto zilizopo, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likitakiwa kuwa kiungo cha uagizaji wa mafuta nchini na kudhibiti uchepushaji.
“Tunaitaka Serikali kuanzisha mfuko maalumu, pindi zinapotokea changamoto kama hizi, tuone namna gani tunaweza kupunguza makali kama hayo,” amesema.
Ametaka kuendelezwa kwa ujenzi wa visima vikubwa vya mafuta, kama vile vya kuhifadhia mafuta vilivyowekewa mawe ya msingi mapema mwaka huu.
Pia ameitaka TPDC kuihamasisha sekta binafsi kuwekeza katika vituo zaidi vya gesi asilia katika mikoa jirani na Dar es Salaam, na ile iliyo mbali wawekeze kwenye LNG.
Aidha, chama hicho tawala kimetaka kuimarishwa kwa utendaji na weledi wa taasisi za Serikali zinazoshughulika na biashara ya mafuta nchini, ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), anayehusika na ununuzi wa mafuta kwa pamoja (bulk procurement) ili kupata bei nafuu.
“Ndugu wananchi, changamoto hii ya kupanda kwa bei ya mafuta si ya Tanzania pekee, bali ni ya kimataifa. Hata hivyo, CCM ina imani kuwa, kwa uongozi thabiti chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, utekelezaji wa sera sahihi na mshikamano wa kitaifa, tutavuka kipindi hiki na kujenga uchumi imara zaidi utakaolinda ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema.
Awali, baada ya kupanda kwa bei ya mafuta Aprili mosi, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alimwagiza Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kujadili mwenendo wa kupanda kwa bei ya nishati hiyo.
Waziri Ndejembi kesho Jumatano akiwa na wataalamu wake watakutana na kamati hiyo ya Bunge kama ambavyo Spika Zungu aliagiza.
Siku hiyo hiyo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alisema Serikali itaketi ili kuangalia uwezekano wa kuleta unafuu kwa Watanzania.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27, Dk Mwigulu alisema: “Tumeona bei zimeshaanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi suala hili ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nzuri na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha.”
Hata hivyo, Dk Mwigulu alisema licha ya changamoto zinazoendelea Mashariki ya Kati, aliwahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa petroli na dizeli, ili kuhakikisha zinaendelea kuwa himilivu.
Wakati hayo yakiendelea, wataalamu wa uchumi wameonya kuwa bila nidhamu ya haraka ya matumizi ya fedha za umma, gharama za mafuta zinazoendelea kupanda zitasababisha kupanda kwa bei za bidhaa na huduma nchini.
Hata wabunge nao, walipochangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu Aprili 2 mwaka huu, waliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza matumizi na kuacha kuendesha mambo kana kwamba hakuna changamoto, kama ilivyoelezwa na mbunge wa Bichosa (CCM), Erick Shigongo.
Mbunge wa Nyasa (CCM), John Nchimbi, alisema eneo la matumizi ya magari ya Serikali linatumia fedha nyingi, akisema ni wakati muafaka liangaliwe upya.
“Iangaliwe aina ya magari yanayotumika na kazi anazozifanya mtumishi. Utakuta mtumishi ni mkurugenzi, tena hapahapa Dodoma, na kazi zake hazimlazimu kutoka nje ya mkoa, lakini anatumia gari la Sh480 milioni.
“Kwa nini anatumia gari la gharama hiyo wakati haendi mbali? Serikali inatumia magari aina ya V8 zaidi ya 400, wakati kuna wengine hawakupaswa kuyatumia hayo,” alisema.
Aidha, Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT Wazalendo), Ado Shaibu, aliitaka Serikali kueleza kwa uwazi maandalizi yake kukabiliana na hali hiyo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alijibu yote hayo, akiwahakikishia wabunge kuwa Serikali iko tayari kuepuka matumizi yasiyo ya lazima, huku ikiendelea kufanya tathmini za mara kwa mara kulinda uchumi.
Mbali na Dk Mwigulu, Aprili 4 mwaka huu, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabili hali hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema wanafanyia kazi jambo hilo kwa umuhimu mkubwa.
“Wataalamu wanachakata namna bora ya kufanya, na wakati wowote Serikali itatoa mwelekeo tutakaochukua. Tunawaomba wananchi wavumilie; muda mfupi ujao watajulishwa,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dk Nasibu Mramba, amesema udhibiti wa matumizi katika taasisi zote za Serikali haukwepeki kwa sasa.
Amesema miradi inayoweza kusubiri iahirishwe hadi hali ya kimataifa itakapokuwa nafuu, huku fedha zikielekezwa katika huduma muhimu za kijamii.
Ameshauri matumizi kama sherehe za kitaifa, ikiwamo Siku ya Muungano, Mei mosi na Sikukuu ya Uhuru, ziahirishwe kwa muda ili kuokoa fedha kwa mahitaji ya dharura.
Mhadhiri mwingine kutoka CBE, Dk Benedict Mwakabungu, amependekeza Serikali ipunguze matumizi ya kawaida, hususan ununuzi wa magari ya kifahari na ya gharama kubwa.
“Kuhusu hatua za muda mrefu, napendekeza, kutokana na kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa duniani, sasa ni wakati wa kuacha kutegemea mafuta pekee na badala yake kutumia fursa ya gesi,” ameshauri.
Kwa upande wa mtaalamu wa sheria na masuala ya kimataifa, Dk Lutengano Mwinuka, amependekeza kuboreshwa kwa ufanisi wa kiutendaji serikalini.
“Nashauri Serikali ipunguze safari zisizo za lazima ndani ya nchi zinazotumia mafuta mengi, ipitie upya sera za kodi kwa bidhaa muhimu kama mafuta, na iongeze uwezo wa hifadhi ya mafuta ya taifa kufikia akiba ya miezi sita hadi 12 ili kukabiliana na mishtuko ya baadaye,” amesema.
Bei hizo za mafuta zimesababisha kupanda kwa nauli katika usafiri wa umma, licha ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kutoa katazo la kupandishwa kwa bei hizo.
Baada ya hali hiyo, Latra imeitisha kikao cha wadau kesho Jumatano, Aprili 8, 2026, jijini Dar es Salaam kupokea maoni yao kuhusu hatua za kuchukuliwa endapo gharama za mafuta zitaendelea kuongezeka.
Wakati hayo yakijiri, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), leo Jumanne, kiliitisha kikao cha kamati ya utendaji kujadili mapendekezo ya nauli watakayowasilisha kesho mbele ya wadau wa usafiri katika kikao cha Latra.
“Ni kweli tumeitisha kikao cha kamati ya utendaji kitakachofanyika leo Jumanne mchana, ajenda ni moja, kuhusu nauli tutakazozipendekeza baada ya mafuta kupanda. Tutakuwa na wahasibu wetu watakaochakata viwango tutakavyopendekeza, kisha kesho tutawasilisha kwenye mkutano,” amesema Mustapha Mwalongo, ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji Taboa.
Hata hivyo, Mwalongo, ambaye ni msemaji wa Taboa, hakuwa tayari kuzungumzia viwango vipya vya nauli watakavyovipendekeza, akisema ni mapema hadi pale watakapomaliza kikao cha kamati ya utendaji ya chama hicho.
Imeandikwa na Katare Mbashiru, Rachel Chibwete (Dodoma), Bakari Kiango na Juma Issihaka (Dar).