SIMBA imepanga kurudi tena katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya kuomba kufanyike marejeo ya shauri lao kumuhusu mchezaji Mohamed Damaro.
Uamuzi huo umekuja baada ya Aprili 2, 2026, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya (TFF) kulitupa shauri la Simba kuhusu uhalali wa kiungo huyo wa Yanga.
Klabu hiyo ilidai usajili wa Damaro umekiuka Kanuni ya 62(1) ya Ligi Kuu pamoja na Kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kamati katika uamuzi wake, ilisema usajili wa Damaro hauna dosari kwa vile habanwi na Kanuni zilizowasilishwa na klabu ya Simba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, amesema leo Jumanne Aprili 7, 2026 kuwa Simba haijaridhishwa na uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kutupilia mbali shauri lao juu ya uhalali wa uraia wa mchezaji huyo, hivyo wanataka kufanyike marejeo ya shauri hilo kabla ya kwenda ngazi za juu zaidi.
“Tumepokea majibu ya kamati ya Hadhi, Sheria za Wachezaji. Tumeshaandaa marejeo ya mchezaji huyu na tutawasilisha hivi punde hapo TFF.
“Na katika hukumu ile waliyotupatia, imechagua tu maeneo yanayowafurahisha ndio wakajibu lakini maeneo mengine tuliyoyahoji hawajayajibu,” amesema Magori.
Magori amesema ameshangazwa kuona Damaro alipata uraia kwa haraka wakati wachezaji wa Simba walikataliwa.
“Mwaka jana na sisi tuliandika barua ya kubadili uraia wa wachezaji wetu lakini haijajibiwa hadi leo. Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa haipo kwenye mizania sawa sio japo sawa. Hili japo sio tu tunakwenda CAS lakini pia tunaiandikia FIFA. Kama mtu anapewa uraia ili tu achezee klabu pekee bila timu ya taifa ni jambo ambalo halikubaliki. Damaro hata ipite miaka 100 hawezi kucheza timu ya Taifa. Jambo lingine ambalo TFF walitakiwa walifanye, kama kanuni zetu halizungumzii hilo basi wangetumia kanuni za juu kufanya maamuzi.
“Hili jambo sio ‘fair’ (sawa) sababu kuna timu moja ina wachezaji 13 kwa kutumia mlango wa nyuma. Na aliyedanganya mamlaka kwamba anapewa uraia ili acheze timu ya taifa basi alifanya udanganyifu mkubwa, unampa uraia wa nini tena mchezaji mwenyewe hana hata mwaka Tanzania. Ni jambo siriazi na sisi tupo nalo siriazi.
“Mashabiki wetu wametaharuki, wamekuwa na hasira, nafahamu mashabiki wetu wanakerwa na hili jambo na wanaona yanayotokea lakini niwasihi sana watulie. Sisi Simba ni timu ambayo inaweka mpira wa miguu mbele. Najua mpira una hasira kubwa. Bodi tunalishughulikia na tumeiandikia mamlaka, tutakutana nao na watatuambia kwanini hayo mambo yanatokea mara kwa mara,” amesema Magori.
Ikumbukwe kuwa, Damaro akiwa Singida Black Stars, alisajiliwa kama raia wa Guinea wakati anatua kikosini hapo Julai 27, 2024, akitokea Hafia ya Guinea, kisha Januari 2025 ilitangazwa alibadili uraia na kupewa wa Tanzania sambamba na Emmanuel Keyekeh wa Ghana na Josephat Bada wa Ivory Coast waliokuwa wote Singida.
Yanga ilipomsajili Damaro wakati dirisha dogo la Januari 2026, ilimchukua kama raia wa Tanzania.
Kutokana na hali hiyo kwa Yanga kumsajili Damaro akiwa Mtanzania na kumtumia bila kuomba kibali cha kubadili uraia wake kwa mujibu wa taratibu za Fifa, kupitia Kamati ya Hadhi ya Wachezaji (Players Status Committee – PSC), imeifanya Simba kufungua kesi TFF ambayo baada ya kusikilizwa, kamati hiyo ililitupilia mbali shauri lao.
Kuhusu Mpanzu ambaye hajaonekana kwenye mechi mbili mfululizo dhidi ya Coastal Union na Azam, kisha kukaibuka madai ya nyota huyo kugoma kutokana na ishu ya maslahi ya mkataba mpya, Magori amesema kila kinachosemwa ni maneno ya kuzusha tu na si vinginevyo.
“Mkataba wake unaisha Septemba 18, 2026, sasa kusema anagoma kwa sababu ya malipo ya mkataba mpya ni suala la ajabu sana, kwanza katika wachezaji wenye nidhamu ni Mpanzu.
“Hii mechi ya Azam FC aliitamani sana lakini anaumwa na anaendelea vizuri na mechi za Arusha kama atakuwa sawa, basi mashabiki watamuona uwanjani.
Wakati huohuo, Magori ameweka wazi ishu ya kiungo raia wa Congo, Inno Loemba akisema: “Kwanza Loemba hajaletwa na JayRutty, alitafutwa na Kamati ya Usajili kwa kushirikiana na kocha. Mkataba wa JayRutty ndio unasema atasajili mchezaji mmoja, ndio tukamwambia alipie gharama zake za usajili, kwani Mohammed [Dewji] anavyosajili wachezaji kwahiyo ni wachezaji wa Mohammed.
“Mkataba wa JayRutty unasema kila mwaka atasajili mchezaji mmoja, hivyo na mwakani mjiandae kuna mchezaji mwingine atalipia gharama za kumsajili.
“Loemba aliumia tangu mechi ya Singida na alianza mazoezi juzi na kocha akamuweka benchi mechi ya Azam. Hakucheza sababu mwalimu aliona bado timu inayocheza ipo vizuri na hakutaka kuchukua risk ya kumchezesha.”