DKT AKWILAPO KUSHIRIKI KONGAMANO LA MIJI AFRIKA NAIROBI

Na Munir Shemweta, Nairobi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt Leonard Akwilapo, anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Kongamano la Pili la Jukwaa la Miji Afrika (2nd African Urban Forum) litakalofanyika kuanzia tarehe 8 hadi 10 Aprili 2026 katika jiji la Nairobi nchini Kenya.

Kongamano hilo linaongozwa na kauli mbiu isemayo “Adequate Housing for All: Advancing Socio-Economic and Environmental Transformation Towards the Realization of Agenda 2063,” linalenga kuhamasisha mijadala itakayotoa fursa kwa washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika kubadilishana uzoefu na suluhisho bunifu katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya miji na makazi.

Kupitia kongamano hilo, Tanzania inatarajiwa kutoa tamko la nchi litakaloeleza jitihada za Serikali katika kuchochea maendeleo endelevu ya miji na makazi, ikiwa ni pamoja na sera, mipango na mikakati inayotekelezwa kuboresha makazi na upangaji wa miji.

Aidha, Mhe. Dkt Akwilapo atashiriki katika mijadala ya ngazi ya juu itakayowahusisha mawaziri, mameya na wataalamu mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya maendeleo ya miji.

Awali Dkt Akwilapo aliongoza kikao cha maandalizi kwa ujumbe wa Tanzania utakaoshiriki kongamano hilo katika ubalozi wa Tanzania nchini Kenya tarehe 7 April, 2026 ambapo masuala mbalimbali ya uwakilishi wa nchi yalijadiliwa.

Dkt Akwilapo ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Deogratias Kalimenze, Mkurugenzi Msaidizi Uzingatiaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi kutoka Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi Bi. Rehema Kishoa, Maafisa kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi pamoja na taasisi binafsi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Kushoto) akimsikiliza kwa makini Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt Bernard Yohana Kibesse (Kulia) kabla ya kuanza kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Kongamano la Miji Afrika litakalofanyika jijini Nairobi kuanzia tarehe 8 hadi 10 April 2026.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akisaini kitabu cha wageni katika ofisi za ubalozi wa Tanzania Nchini Kenya mara baada ya kuwasili ubalozini katika kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Kongamano la Miji Afrika litakalofanyika jijini Nairobi kuanzia tarehe 8 hadi 10 April 2026.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akioongoza kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Kongamano la Miji Afrika kwa ujumbe wa Tanzania katika ubalozi wa Tanzania jijini Nairobi tarehe 7 April 2026.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Balozi Dkt Bernard Yohana Kibesse akizungumza katika kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Kongamano la Miji Afrika litakalofanyika jijini Nairobi kuanzia tarehe 8 hadi 10 April 2026. Kushoto ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo na Kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Bw, Deogratias Kalimenze.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akisaini kitabu cha wageni katika ubalozi wa Tanzania nchini Kenya. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe Balozi Dkt Bernard Yohana Kibesse na Katikati ni Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya Bi Eliet Magogo (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).