Huduma za upasuaji ni moja ya huduma muhimu za tiba. Ni huduma zinazotokana na maendeleo ya sayansi duniani na leo tunapoadhimisha Siku ya Afya Duniani ninapenda tuziangazie huduma hizi adhimu.
Afya ni msingi wa maendeleo, na huduma za upasuaji ni sehemu muhimu ya huduma hizi adhimu.
Hapa Afrika, hata katika tiba za jadi za zamani za kale, bado huduma za upasuaji zilitolewa, kwa mfano huduma za uzazi salama na kufunga mifupa iliyovunjika.
Tiba za upasuaji ni sayansi inayoishi inayotumia teknolojia na ujuzi kuondoa sehemu inayoumwa au chanzo cha matatizo kwa kufanya upasuaji mahususi kwa kutumia vifaa maalumu kama mikasi n.k.
Hapa nchini hospitali haikamiliki wala haipati usajili ikiwa hakuna vyumba na wodi za upasuaji. Hivyo ni kusema hakuna hospitali kama hakuna huduma za upasuaji.
Magonjwa mengine ni kweli hutibiwa kwa dawa za kumeza na mengine kwa sindano. Hata hivyo, bado yako magonjwa mengine yanayotibiwa kwa njia ya upasuaji.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria watu bilioni tano duniani hawapati huduma za upasuaji salama, na wengine hutumia gharama kubwa tena pesa taslimu kutoka mfukoni ili kupata huduma hizi adhimu huku wakiachwa katika wimbi la umaskini wa kutupa. Yaani, endapo mtu atatakiwa kufanyiwa upasuaji hulazimika kuuza mali kama vile shamba na mifugo ili kupona.
Nchini Tanzania, asilimia 20 ya vifo vyote hutokana na magonjwa ambayo yangetibiwa kwa upasuaji.
Maendeleo ya sayansi yamebadili namna upasuaji unavyofanyika. Zamani watu walifanyiwa upasuaji bila kutakasa vyombo. Hivi sasa, vyombo hutakaswa kwa teknolojia ya hali ya juu na imeboresha mno matokeo ya huduma za upasuaji.
Teknolojia za kisasa za upasuaji, kwa kutumia vifaa vya kuzuia damu kuvuja na kuunganisha utumbo kwa kutumia vifaa maalumu kama stapler, zimepunguza muda wa kufanya upasuaji.
Upasuaji kwa matumizi ya kamera, kupitia matundu madogo na matundu asilia, umefanya upasuaji mwingi kuwa na matokeo mazuri na kufanya muda wa kupona kuwa mfupi.
Upasuaji wa tezi dume kwa kutumia teknolojia ya telescope (TURP) kupitia njia ya mkojo umerahisisha mno na kupunguza muda wa kusubiri kidonda kipone hospitalini. Kwa sasa kuna teknolojia ya kutumia mionzi maalumu ya laser au mvuke (Rezūm).
Hivi karibuni, teknolojia ya upasuaji kwa kutumia roboti imeshika kasi. Hivi karibuni, mgonjwa akiwa China alifanyiwa upasuaji wa moyo kwa kutumia roboti, huku daktari wa upasuaji akiwa nchini Ufaransa.
Mambo yanaenda kasi. Upasuaji wa dharura kumtoa mtoto kwa sasa unafanyika katika vituo vya afya. Tiba za mifupa iliyovunjika zinafanyika kwenye hospitali za mikoa na kanda. Operesheni za moyo na ubongo nazo zinafanyika hapa nchini.
Kwa sasa, upasuaji wa dharura ni sehemu ya huduma za msingi. Pia operesheni za kurekebisha viungo vilivyoharibika kutokana na jeraha au kuzaliwa na maumbile yasiyosawia ni kitu cha kawaida. Hata upasuaji rekebishi na wa urembo ni huduma inayopatikana hapa nchini pia.
Huduma za upasuaji huhitaji huduma dhabiti, zikiwemo huduma za usingizi tiba (anaesthesia). Hakuna upasuaji salama kama hakuna huduma za usingizi tiba salama.
Mgonjwa akitoka chumba cha upasuaji huhitaji uangalizi maalumu ICU au wodi za kawaida, hivyo wauguzi ni sehemu muhimu ya huduma hizi za upasuaji.
Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani lilipitisha azimio namba 68:15 lililolenga kuimarisha huduma za upasuaji ulimwenguni. Azimio hili lilizitaka nchi wanachama kuongeza uwekezaji kwenye huduma za upasuaji.
Azimio hili linazitaka nchi wanachama kuhakikisha huduma za upasuaji ni sehemu muhimu ya mpango wa afya kwa wote.
Azimio hili linaweka matakwa ya kuondoa vikwazo kwa wananchi kufikia huduma za upasuaji.
Nchi yetu ya Tanzania ni sehemu ya azimio hili, na iliandaa mpango kabambe wa kuimarisha huduma za upasuaji (NSOAP) uliotekelezwa tangu mwaka 2018–2026.
Mpango huu ulilenga kuongeza wigo wa huduma za upasuaji, idadi ya vyumba vya upasuaji, madaktari wa upasuaji na uwekezaji wa kimkakati katika huduma za upasuaji nchini Tanzania.
Siku hii ya Afya Duniani tunaadhimisha uwepo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) linalohamasisha uwekezaji katika sekta ya afya. Pia, tunatumia fursa hii kufurahia mafanikio tuliyoyapata tangu kuanzishwa kwake. Tunatumia siku ya leo pia kutafakari maazimio na hali ya utekelezaji wa mipango iliyoanzishwa na WHO kitaifa, kikanda na kiulimwengu.
Hata hivyo, bado kuna changamoto zinazotukabili na hatuna budi kuendelea kutafakari na kubuni njia za kuzitatua. Nina hakika kwa utashi madhubuti, ushirikishwaji wa wananchi na mikakati mtambuka tutafikia malengo tuliyojiwekea.
Bado imani ya wananchi katika huduma za upasuaji iko hafifu. Wengi ni waoga na wanachelewa kufika hospitalini kujipatia huduma za upasuaji.
Tanzania na kwingineko Afrika, hospitali bado zina madaktari na wahudumu wa afya wachache, vifaa vya upasuaji havipatikani kwa urahisi na wananchi bado wanakumbana na gharama wanapotaka huduma za upasuaji.
Siku ya leo tunawakumbusha wadau wote kuziangazia huduma za upasuaji nchini na kuongeza uwekezaji ili kila anayehitaji huduma hizi azipate kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa usalama.
Tunatoa rai kwa Serikali kuchunguza maendeleo ya huduma za afya, hususani za upasuaji kwa wote.
Tunapoungana kwa pamoja kuadhimisha Siku ya Afya Duniani, tunajikumbusha kuzingatia matumizi ya sayansi za tiba za upasuaji kama sehemu muhimu ya huduma za afya na sehemu maalumu ya huduma za afya kwa wote.
Mwandishi ni Daktari Bingwa wa Upasuaji, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).
