Dar es Salaam. Sakata la kuungua kwa Soko la Simu 2000, Ubungo jijini Dar es Salaam limeibua mahitaji tofauti miongoni mwa wafanyabiashara; wapo waliodai wako tayari kurudi sokoni hata kwa mitaji midogo iliyosalia, huku wengine wakisubiri huruma ya Serikali.
Wakati wafanyabiashara wakiwa na mahitaji hayo tofauti, Serikali haijaweka wazi ni lini itatoa ruhusa kwa shughuli za biashara kuendelea kufanyika katika soko hilo, lililoungua moto Aprili 4, mwaka huu.
Hata hivyo, tayari shughuli za usafi sokoni hapo zinakaribia kukamilika, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Aprili 6, 2026 la Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyetaka usafi ufanywe haraka ili shughuli ziendelee.
Mwananchi ilifika katika soko hilo leo Jumanne, Aprili 7, 2026 saa 4 asubuhi na kushuhudia utekelezaji wa agizo hilo ukiwa katika hatua za mwisho.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipokagua madhara yaliyotokana na kuungua kwa soko la wafanyabiashara wadogo la Simu 2000, lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Tayari mabaki yote ya vibanda vilivyoteketezwa kwa moto yalikuwa yameondolewa katika eneo hilo, huku magari yakimalizia kuondoa uchafu katika maeneo hayo.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi wamepongeza utekelezaji wa haraka wa maagizo hayo huku wakiiomba mamlaka kuharakisha mchakato wa utambuzi wa wafanyabiashara katika eneo hilo na kuwa uwe wa haki.
Pia wameomba kupatiwa mikopo kukufua mitaji yao, kwani baadhi yao bidhaa zao zote ziliteketea katika ajali hiyo.
Wengine wamesema wapo tayari kuanza biashara; wanachosubiri ni maelekezo kutoka kwa mamlaka husika kuhusu lini wanaweza kuendelea na biashara katika eneo hilo.
Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo, Saidi Daudi, anasema pamoja na usafishaji kufanyika haraka, ameshauri pia mchakato wa kuwezeshwa kupata mikopo ufanyike kwa haraka ili waweze kupata mitaji na kuendelea na biashara zao.
“Baada ya biashara yangu kuteketea, maisha yangu yamekwama. Sijui nitalipaje mikopo wala kuendesha maisha yangu,” amesema.
Mmoja wa wafanyabiashara aliyekuwa akifanya shughuli zake katika Soko la Simu 2000, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, anasema yuko tayari kurejea katika biashara yake; anachosubiri ni maelekezo ya lini wanaweza kuanza.
“Maji yameshamwagika hayawezi kuzoleka tena. Bidhaa zangu zimeshateketea, inauma lakini kuendelea kuhuzunika hakutanisaidia. Tutakaporuhusiwa kuendelea na biashara zetu, mimi nipo tayari kuanza na kidogo nilichonacho,” amesema.
Kwa upande wake, mfanyabiashara ambaye naye aliathirika na tukio hilo, Tumpesifa Mwakasege amesema yuko tayari kurejea na kuendelea na biashara lakini kinachomuumiza kichwa ni wapi atapata mtaji.
Tumpesifa, ambaye alikuwa akijishughulisha na uuzaji wa nguo, amesema siku ya tukio la moto ilikuwa ndiyo siku aliyokuwa amekusanya akiba yake yote na kununua bidhaa mpya.
“Ninatamani kuendelea na biashara lakini sina pa kuanzia. Mtaji na akiba zangu zote ziliteketea katika ajali ile. Natamani mchakato wa halmashauri kutuwezesha ungeharakishwa ili tuweze kupata mitaji na kurejea katika biashara,” amesema.
Tayari Waziri Mkuu amesisitiza usimamizi thabiti katika ugawaji wa vizimba katika soko lolote ili kuhakikisha wanaopewa ni wanaomiliki biashara.
Dk Mwigulu amesema baadhi ya watu wamegeuza fursa za biashara kuwa njia ya kujinufaisha bila kufanya kazi, jambo ambalo ni kinyume na taratibu na linawaumiza wengine.
“Wapo wanaochukua maeneo hawafanyi biashara; wanakaa kama walanguzi, wanaweka chazo cha ziada, wanakodisha kwa wengine na kuongeza gharama kwa wafanyabiashara wadogo. Hii haikubaliki hata kidogo,” alisema.
Kwa upande wa wafanyabiashara waliopata hasara au waliokuwa na mikopo, Waziri Mkuu aliagiza uongozi wa mkoa na wilaya kukusanya taarifa zao na kushirikiana na taasisi za kifedha ili kupata suluhisho la haraka.
“Pateni orodha ya wote walioathirika, mjue wamekopa wapi, tuzungumze na taasisi husika ili wapate nafuu na waweze kuendelea na biashara zao,” amesema.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipokagua madhara yaliyotokana na kuungua kwa soko la wafanyabiashara wadogo la Simu 2000, lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Katika kupunguza makali ya hasara, Dk Mwigulu aliielekeza halmashauri ya wilaya ya Ubungo kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya uwezeshaji zinatolewa kwa wafanyabiashara hao ili kuwasaidia kurejea kwenye shughuli zao bila kuchelewa.
Alisisitiza kuwa hakuna sababu ya ucheleweshaji wakati tayari kuna wafanyabiashara walioathirika na wanaohitaji mtaji wa kuanza upya.
“Fedha hizi zipo kwa ajili ya wananchi, si za kukaa kwenye akaunti. Toeni kwa haraka kwa wale waliostahili ili waweze kurejea kwenye biashara zao,” alisema.
Alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri kupitia mifumo ya mikopo na kuhakikisha wale waliopata hasara wanapewa kipaumbele katika mgao huo.
