Global Publishers
April 8, 2026
0 Comments
Marekani imeendelea na operesheni zake za kijeshi dhidi ya Iran baada ya kuripotiwa kushambulia maeneo ya kijeshi katika Kisiwa cha Kharg, eneo linalojulikana kwa umuhimu wake katika usafirishaji wa mafuta duniani. Hatua hiyo imeibua mjadala mpya kuhusu mwelekeo wa mgogoro kati ya mataifa hayo mawili.
Akizungumza mjini Budapest, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesisitiza kuwa mashambulizi hayo hayaashirii mabadiliko yoyote ya mkakati wa Marekani katika mgogoro huo. Amesema kuwa operesheni hiyo ililenga maeneo ya kijeshi pekee na si miundombinu ya nishati au mafuta.
Kwa mujibu wa Vance, Marekani bado inaamini kuwa njia ya mazungumzo yanaendelea, huku ikitarajia Iran kutoa majibu ya mapendekezo ya suluhu ndani ya muda uliowekwa. Amesema pia kuwa Marekani haitalenga miundombinu ya nishati hadi pale Iran itakapokubali kushiriki mazungumzo yenye tija au kutoa mapendekezo yanayokubalika.
Afisa mmoja wa Marekani aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema kuwa baadhi ya maeneo yaliyoshambuliwa tayari yalishawahi kulengwa hapo awali, na kwamba mashambulizi hayo yalifanyika katika saa za asubuhi.
Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kusisitiza Iran kuachana na mpango wa silaha za nyuklia pamoja na kufungua tena Strait of Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.