Bagamoyo. Jengo la Mahakama ya Lugoba lililopo Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani, limeteketea kwa moto usiku wa Aprili 6, 2026, huku chanzo cha tukio hilo kikiwa hakijajulikana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, tukio hilo lilitokea majira ya saa 2:30 usiku na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na nyaraka muhimu zilizokuwa ndani ya jengo hilo.
“Ni kweli kumetokea ajali ya moto katika Mahakama ya Lugoba ambapo jengo lote limeteketea. Hata hivyo, hakuna madhara ya kibinadamu yaliyoripotiwa na uchunguzi wa chanzo cha moto unaendelea,” amesema Morcase.
Amesema baada ya kupokea taarifa hizo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Tanesco walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti moto huo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wenye taarifa zitakazoweza kusaidia kubaini chanzo cha tukio hilo kujitokeza ili kusaidia uchunguzi unaoendelea.
“Tunaomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kubaini chanzo cha tukio hili kwa haraka zaidi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Pwani wamesema tukio hilo limeibua hofu kuhusu usalama wa majengo ya umma, hususan yale yanayohifadhi nyaraka nyeti za kisheria.
Mkazi mmoja, Juma Mwalimu, amesema matukio ya moto yanapotokea mara kwa mara yanazua wasiwasi na kuhoji uimara wa mifumo ya ulinzi katika taasisi muhimu za Serikali.
“Serikali inapaswa kuimarisha mifumo ya usalama katika majengo muhimu kama mahakama ili kulinda nyaraka na haki za wananchi,” amesema.
Kwa upande wake, Halima Rashid amesema kupotea kwa nyaraka hizo kunaweza kuwa na athari kwa wananchi wenye mashauri mahakamani.
“Wapo watu wanaofuatilia kesi zao, sasa nyaraka zinapoteketea inaweza kuchelewesha au kuathiri haki zao,” amesema.
