Sakata la Uraia Lapamba Moto, Simba Yagoma Kukubali Uamuzi – Video

Global Publishers
April 8, 2026
0 Comments

Klabu ya Simba SC imesisitiza kuwa bado haijafunga ukurasa wa sakata la mchezaji wa Yanga, ikionesha nia ya kuendelea kulifuatilia suala hilo hadi mwisho wake.

Hatua hiyo inakuja licha ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Tanzania Football Federation (TFF) kutupilia mbali malalamiko ya Simba yaliyohusu uraia wa mchezaji huyo. Uamuzi huo haujaizima Simba, ambayo sasa imeamua kuwasilisha upya maombi ya marejeo kwa shirikisho hilo.

Akizungumza kwa niaba ya klabu hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema wazi kuwa hawatarudi nyuma katika kuhakikisha wanapata haki wanayoamini ipo upande wao.

“Tumewasilisha upya suala hili TFF kwa ajili ya marejeo. Ikitokea hatutapata majibu ya kuridhisha, tuko tayari kulipeleka suala hili katika vyombo vya juu zaidi vya mpira duniani,” amesema Magori.

Simba inaamini kuwa kuna maswali ambayo hayajajibiwa kikamilifu kuhusu uhalali wa mchezaji huyo, jambo linalowasukuma kuendelea kupigania kile wanachodai ni haki yao ndani na nje ya uwanja.

Endapo jitihada zao ndani ya TFF hazitazaa matunda, klabu hiyo imeweka wazi kuwa ipo tayari kwenda katika Mahakama ya Kimataifa ya Michezo, Court of Arbitration for Sport (CAS), au hata kufikisha suala hilo kwa FIFA.

Sakata hilo linaendelea kuvuta hisia za mashabiki wa soka nchini, hasa kutokana na ushindani mkubwa uliopo kati ya Simba na Yanga, huku wengi wakisubiri kuona hatma ya mgogoro huo ambao sasa unaonekana kuelekea katika ngazi za kimataifa.