Sebo aendeleza rekodi mbovu kwa Singida Black Stars

BEKI wa kati wa Singida Black Stars, Abdallah Kheri ‘Sebo’, amekuwa mchezaji wa pili wa timu hiyo msimu huu kujifunga dhidi ya TRA United, akiendeleza rekodi mbovu kwa kikosi hicho katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Katika mechi iliyochezwa Jumapili Aprili 5, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, Sebo alijifunga dakika ya tisa akiwa katika harakati za kuokoa, kisha Christopher Tebandeke akafunga bao la pili kwa penalti dakika ya 40 na TRA kushinda mabao 2-0.

Sebo aliyejiunga na Singida dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Pamba Jiji, amekuwa mchezaji wa pili wa timu hiyo kujifunga katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya TRA United, baada ya awali kumtokea pia beki, Anthony Tra Bi Tra ambaye tayari ameachana na Singida Black Stars kipindi cha dirisha dogo.

Katika mechi ya raundi ya kwanza msimu huu ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Desemba 6, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam,  Anthony Tra Bi Tra alijifunga dakika ya 87, Singida ikichapwa mabao 3-1.

Wakati Tra Bi Tra akijifunga, mabao mengine ya TRA yalifungwa na Chanda Chewe dakika ya 10 na Shaaban Idd Chilunda dakika ya 82, huku la Singida likifungwa na Clatous Chama kwa penalti ya dakika ya 54, hivi sasa kiungo huyo yupo Simba.

Baada ya Tra Bi kujifunga, imemchukua Sebo takribani siku 121 naye kujifunga dhidi ya TRA United, huku msimu huu timu hiyo ikivuna pointi zote sita, zilizosababisha pia benchi lote la ufundi la Singida Black Stars kuvunjwa kutokana na mwenendo usioridhisha.

Singida ililivunja benchi la ufundi, likiongozwa na Mkenya David Ouma, aliyeteuliwa Januari 5, 2026, akichukua nafasi ya Miguel Gamondi, aliyejiunga na timu ya taifa ya Taifa Stars na aliyekuwa meneja wa kikosi hicho, Mtunisia Othmen Najjar.

Sebo aliyetamba na timu za JKU SC, Zimamoto zote za Zanzibar na Ndanda, bado ni mchezaji halali wa Azam FC na baada ya msimu huu kuisha ndipo mkataba wake utafikia tamati, hivyo Singida itaamua imsajili moja kwa moja au iachane naye.