Dar es Salaam. Wakati makali ya bei ya mafuta yakiendelea kung’ata, Serikali imesema muda utakapofika itatoa taarifa ya hatua ilizochukua kuleta ahueni ya gharama ya nishati hiyo kwa wananchi.
Serikali inakuja na ahadi hiyo katika kipindi ambacho mataifa mengine Afrika yameshachukua hatua, huku mengine yakiwa kwenye mchakato wa hatua, kama ilivyo kwa Tanzania.
Akizungumzia hatua zilizofikiwa hadi sasa, siku tano baada ya tamko la Waziri Mkuu, Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio, amesema taarifa itatolewa wakikamilisha utaratibu.
“Waziri Mkuu ameshatoa maelekezo, muda ukifika tutawaeleza Watanzania,” amesema Dk Matarahio alipizungumza na Mwananchi leo, Aprili 6, 2026 kisha kukata simu.
Machi 31 mwaka huu, Serikali ya Afrika Kusini ilitangaza kupunguza ushuru kwa kiasi cha randi 3 (sawa na Sh454.74) katika kila lita moja ya mafuta kwa kipindi cha mwezi mmoja, ikiwa ni hatua ya kudhibiti mfumuko wa bei.
Kwa upande wa Taifa la Mauritania, ambako bei ya mafuta imepanda kwa asilimia 15.3 kwa petroli na asilimia 10 kwa dizeli, limetangaza hatua ya kutoa msaada wa kifedha kwa familia duni, angalau kuziwezesha kumudu gharama za maisha.
Serikali ya Zambia imetangaza kupunguza makali ya bei ya mafuta kwa kuondoa baadhi ya kodi muhimu kwa miezi mitatu kuanzia Aprili mosi, mwaka huu. Zambia imeidhinisha kuondolewa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 16, ushuru wa bidhaa na ushuru wa forodha ili kushusha gharama.
Hatua hiyo ya Serikali ya Zambia inatajwa kupunguza bei ya nishati hiyo kwa asilimia 13.8, huku ushuru wa bidhaa ukichangia punguzo la takribani asilimia 15.
Kwa upande wa Tanzania, tayari Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema suala hilo linafanyiwa kazi.
“Tumeona bei zimeshaanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi suala hili ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nzuri na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha,” alisema alipokuwa akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2026/2027.
Katikati ya michakato hiyo ya Serikali, wataalamu wa uchumi wamependekeza kuongeza uzalishaji wa gesi na matumizi yake, kuweka ruzuku kwenye mafuta, na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuangalia upya zana zake za kifedha, pamoja na mapitio ya kodi na tozo ili zipunguzwe.
Hayo yanakuja baada ya kupanda kwa bei ya mafuta kulikosababishwa na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, vikihusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Hatua hiyo imesababisha baadhi ya visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na viwanda vya kusafisha mafuta kushambuliwa, huku lango la Hormuz, linalopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa kwenda kwenye masoko mbalimbali duniani, likifungwa.
Kutokana na hali hiyo, wanunuaji wa petroli kwa bei ya rejareja inayopitia Bandari ya Dar es Salaam watalazimika kuongeza Sh956 katika kila lita moja ya mafuta baada ya bei kufikia Sh3,820 kutoka Sh2,864.
Kwa upande wa dizeli, lita moja sasa itanunuliwa kwa Sh3,806 kutoka Sh2,858, ikiwa ni ongezeko la Sh948, huku mafuta ya taa sasa yatanunuliwa kwa Sh3,684 kutoka Sh2,932.
Kwa wanaonunua petroli inayopitia Bandari ya Tanga, wataendelea kuathirika zaidi, kwani sasa lita moja itauzwa kwa Sh3,881 kutoka Sh2,925, ikiwa ni ongezeko la Sh956 kwa kila lita.
Wanaotumia mafuta ya dizeli yanayopita katika bandari hiyo sasa watanunua lita moja kwa Sh3,867 Aprili mwaka huu kutoka Sh2,919 ya Machi, ikiwa ni ongezeko la Sh948 kwa lita. Wale wa mafuta ya taa nao watalazimika kuongeza Sh752 kwa kila lita baada ya mafuta kufikia Sh3,745 kutoka Sh2,993.
Wakazi wa Mtwara ndio wenye makali zaidi kuliko wengine wote. Lita moja ya petroli inauzwa kwa Sh3,912, ikiwa ni ongezeko la Sh956 kutoka bei ya Machi mwaka huu. Mafuta ya dizeli nayo yamefikia Sh3,898 kutoka Sh2,951, ikiwa ni ongezeko la Sh947, huku mafuta ya taa yakifikia Sh3,777 kwa lita kutoka Sh3,025, ikiwa ni ongezeko la Sh752.
Akizungumzia namna ya kupunguza matumizi ya Serikali na machungu kwa wananchi, mchambuzi wa sera za uchumi, Dk Baraka Mrosso, amesema anaamini Tanzania inaweza kuiga mfano wa Kenya, lakini kwa tahadhari.
“Ruzuku ya mafuta inaweza kuwa suluhisho la muda mfupi, hasa kwa sekta nyeti kama usafiri wa umma na kilimo, lakini ni lazima kuwe na tahadhari ili isilete mzigo katika bajeti ya Serikali,” amesema.
Kwa upande wa mchambuzi wa uchumi, Profesa Neema Kalinga, amesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaweza kutumia zana zake za kifedha kuongeza riba ili kupunguza mfumuko wa bei.
“BoT inaweza kutumia zana zake za kifedha kama kuongeza riba kwa kiwango cha tahadhari, ili kupunguza mfumuko wa bei. Lakini hatua hii inahitaji mizani ili isikandamize ukuaji wa uchumi,” ameeleza.
Mtaalamu wa masuala ya nishati, Rashid Mwakyusa, amesema suluhisho la kudumu liko katika uzalishaji wa ndani.
“Tanzania ina gesi asilia ya kutosha. Tunapaswa kuharakisha uwekezaji katika kusafisha na kutumia gesi hiyo kwa matumizi ya viwandani na usafiri. Hii itapunguza utegemezi wa mafuta ya nje,” amesisitiza.
Kwa hatua iliyofikia sasa, Mwakyusa amesema Serikali inapaswa kuongeza ulinzi kwa makundi yenye kipato cha chini ili yamudu gharama za maisha.
“Kupanda kwa bei ya mafuta kunaathiri zaidi wananchi wa kipato cha chini. Serikali inaweza kuwapa wananchi hawa chakula na uwezeshaji wa kifedha, ili kuwasaidia kupunguza makali ya hali hii,” amesema.
Mtaalamu wa biashara, Kelvin Mhando, amesisitiza umuhimu wa kuangalia sera za kodi ili kupunguza tozo na kodi kwenye nishati hiyo.
“Kupunguza baadhi ya tozo na kodi kwenye mafuta kwa muda kunaweza kusaidia kushusha bei. Pia ni muhimu kupanua wigo wa mapato ya Serikali ili kufidia upungufu huo,” amesema.
Katika upande wa familia, Dk Donald Mmari amesema ni vyema kuangalia namna ya kupunguza matumizi, ikiwemo kuepuka safari zisizo za lazima.
“Kwa sababu bei imepanda, waangalie kufanya zile zinazoonekana kuwa za muhimu zaidi. Pia waangalie namna mpya ya kuweka vipaumbele katika bajeti zao ili kuendana na hali za sasa,” amesema.
Kwa upande wa Serikali, amesema ni wakati wa kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi kwenye mafuta ili bei zishuke na kutoa ahueni kwa wananchi, ingawa hatua hiyo itapunguza mapato ya Serikali, hivyo kulazimika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Wakati haya yakiendelea, viwanda vitano vya utengenezaji wa magari yanayotumia nishati safi vimesajiliwa nchini katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tiseza), Gilead Teri, amesema mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati yameanza kuleta athari chanya kwa Tanzania, kwani wawekezaji wengi sasa wanatafuta maeneo mbadala yenye utulivu.
Amesema Tanzania imekuwa chaguo muhimu kutokana na mazingira yake rafiki ya uwekezaji.
“Hii inaonesha mwelekeo mpya wa uwekezaji katika nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira. Tunaona wazi Tanzania inaanza kuwa kitovu cha uwekezaji katika sekta hii ndani ya ukanda,” amesema.
