Dar es Salaam. Wizara ya Afya imetangaza kuanza msako kwa wauzaji wa bidhaa za afya hususan vipodozi na dawa zisizosajiliwa mitandaoni huku Shirika la Viwango Tanzania (TBS) likitaja vigezo vinavyopaswa kufuatwa ili bidhaa iwe halali kuuzwa sokoni.
Hatua hiyo imeelezwa ni sehemu ya kulinda afya za wananchi dhidi ya matumizi ya bidhaa zisizo salama, wakati matumizi ya mitandao ya kijamii yakiendelea kuwa njia rahisi ya uuzaji wa bidhaa hizo bila udhibiti wa kutosha.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 7, 2026 na Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Dk Rahma Hingora wakati akiendesha mjadala wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani yaliyobeba ujumbe usemao, “Pamoja tutumie sayansi, kwa manufaa yetu sote.”
Msakako huo wa vipodozi na dawa zisizosajiliwa unatolewa takribani wiki mbili tangu Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa kuitaka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuwachukulia hatua mtu yeyote atakayejitangaza kutoa huduma za tiba asili bila kusajiliwa.
Waziri huyo alisema lazima watu hao watambuliwe kwa kusajiliwa kwenye jumuiya za watafiti na watoa huduma za tiba asili. Akigusia wapo watu wanaoibuka wakisema ‘ukipata changamoto ya figo fanya hivi usiende hospitali’ haiwezekani.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Dk Rahma Hingora akizungumza wakati akiendesha mjadala huo katika maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani yaliyobeba ujumbe usemao, “Pamoja tutumie sayansi, kwa manufaa yetu sote”.
“Kama ni madaktari wawe wanatambulika na kama ni watoa huduma za asili lazima watambuliwe ili yule anayetoka akizungumzia tiba fulani tuwe tunamtambua. Haiwezekani tukawa na Taifa ambalo kila mtu anasimama anasema yeye ni daktari, anatibu hiki na hiki,” alisema Mchengerwa, Machi 25, 2026 katika mkutano wake na watoa huduma wa tiba asili.
Katika suala la vipodozi na dawa, Dk Hingora amesema taarifa potofu zimekuwa tishio, zikichangia watu kufanya uamuzi hatarishi kuhusu afya zao, ikiwemo kutumia dawa zisizo sahihi au kuamini tiba zisizothibitishwa kisayansi.
Amesema mitandao ya kijamii inapaswa kutumika kwa kutoa elimu sahihi ya afya badala ya kuwa jukwaa la kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho wa kitaalamu.
Amesema ni muhimu kwa bidhaa za ngozi na afya kwa ujumla kuzungumziwa na wataalamu waliothibitishwa, huku akisisitiza Serikali ipo mbioni kufuatilia kwa kina biashara hizo ili kuhakikisha bidhaa zote zinazopatikana sokoni zimefanyiwa uchunguzi wa kisayansi na kuidhinishwa na TBS.
“Tutalitilia mkazo jambo hili. Hata mtu anayetoa elimu ya afya lazima afuate taratibu na awe na kibali maalumu,” amesema Dk Hingora.
Mwananchi iliwatafuta TBS kutaka kujua ni vigezo gani vinatakiwa kabla ya bidhaa kuingizwa nchini na hapa Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Habakuki Kalebo amesema kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Sura ya 130, mfanyabiashara yeyote anayetaka kuingiza au kuuza vipodozi au bidhaa za chakula lazima asajiliwe rasmi kama muingizaji na pia kuhakikisha bidhaa zake zimesajiliwa.
Ameeleza bidhaa hupitia tathmini ya kina ikiwemo uchunguzi wa viambata vyake na kupimwa maabara ili kubaini kama vinakidhi viwango vya ubora na usalama kwa matumizi ya binadamu.
“Ni lazima mfanyabiashara ajulikane anaingiza nini, anakipeleka wapi, anakihifadhi vipi na anakisambaza kwa njia ipi. Bidhaa inapimwa kabla ya kupewa cheti cha ubora ambacho hudumu kwa muda maalum,” amesema Kalebo.
Ameongeza hata baada ya kusajiliwa, kila mzigo unaoingizwa nchini hupaswa kukaguliwa upya ili kuhakikisha unakidhi viwango vilivyowekwa.
Habakuki amesema zipo bidhaa mtandaoni ambazo zinauzwa na huingizwa kwa njia ya panya, TBS imekuwa ikiwakamata wafanyabiashara hao na kuwachukulia hatua.
“Tunakagua maeneo yote lazima tuhakikishe hizo bidhaa zimesajiliwa huwa tunakagua, tukizikuta zinaondolewa kutoka sokoni mpaka azisajili ndiyo utaratibu iwe anauzia mtandaoni au wapi. Lazima bidhaa isajiliwe, muuzaji asajiliwe na eneo analotunzia bidhaa lisajiliwe.
“Matangazo yoyote ya mtandaoni lazima yawe yamepewa kibali, tumekuwa tukikutana nao na kuwachukulia hatua,” amesema habakuki.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wameonya kuongezeka kwa taarifa za matangazo ya vipodozi na matibabu yasiyo na uthibitisho wa kisayansi yanayosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, wakisema mwenendo huo unahatarisha afya ya umma.
Kwa mujibu wa WHO, kila mafanikio ya afya tunayoyaona leo yanatokana na utafiti wa kisayansi uliothibitishwa kwa ushahidi.
Lakini utafiti wa mwaka 2025 kuhusu mitandao ya kijamii ulibaini kuwa, taarifa potofu za afya husambaa kwa kasi kubwa kupitia mitandao ya kijamii, huku watu wachache wenye ushawishi wakiweza kueneza sehemu kubwa ya taarifa hizo.
Ongezeko la taarifa zisizo sahihi mtandaoni linahatarisha mafanikio hayo kwa kupunguza imani ya jamii kwa wataalamu wa afya na mifumo rasmi ya huduma.
“Katika dunia inayokabiliwa na changamoto nyingi za kiafya, tunahitaji kusimama na sayansi kwa kuzingatia ushahidi, ukweli na mwongozo wa kitaalamu,” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus katika taarifa yake ya maadhimisho ya mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkaazi wa WHO Tanzania, Dk Alex Gasasira
Wakati wa mjadala huo, Dk Hingora amesema Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kufuata sayansi katika kulinda afya, akihusisha juhudi hizo na kaulimbiu ya mwaka ya “One Health” inayounganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Kwa mujibu wake, magonjwa ya mlipuko kama Marburg Virus Disease na Mpox yanaonesha umuhimu wa ushirikiano huo, kwani mengi hutokana na mwingiliano kati ya binadamu, wanyama na mazingira.
Mkurugenzi wa Kukuza na Kuratibu Tafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania, Dk Nyanda Ntinginya, amesema taasisi hiyo imeendelea kuzalisha ushahidi wa kisayansi kwa zaidi ya miongo minne na nusu ili kusaidia kuboresha sera na mifumo ya afya nchini.
Amesema NIMR inashirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kufanya tafiti na kutafsiri matokeo yake ili yaweze kutumika katika kufanya maamuzi sahihi ya kiafya.
Mkurugenzi wa Kiufundi wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani kutoka CIHEB Tanzania, Dk Siril Kullaya amesema takribani asilimia 60 hadi 70 ya magonjwa ya mlipuko yanatokana na wanyama na mazingira.
Amesisitiza kuwa matumizi ya mkakati wa “Afya Moja” yanawezesha kugundua na kudhibiti magonjwa mapema kabla hayajaenea kwa binadamu, huku akibainisha kuwa ushirikiano kati ya sekta za afya ya binadamu, mifugo na mazingira ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hizo.
“Afya na uchumi vinaenda pamoja. Tukishirikiana vizuri kama Taifa, tutaimarisha usalama wa afya na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” amesema Dk Kullaya.
Akizungumza kupitia ujumbe wake rasmi, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika WHO, Dk Mohamed Janabi amesema kaulimbiu ya mwaka huu, “Pamoja kwa afya. Simama na sayansi”, inaakisi mchango mkubwa wa tafiti za kisayansi katika kuokoa maisha na kuboresha huduma za afya duniani.
Amesema jitihada za afya ya umma zinazotegemea ushahidi wa kisayansi zimeleta mafanikio makubwa, hata hivyo, amebainisha kuwa bado Afrika inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo magonjwa sugu, milipuko mipya ya magonjwa na mifumo dhaifu ya afya.
Ameeleza kuwa mkakati wa Afya Moja unaohamasisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali umesaidia nchi nyingi za Afrika kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, tathmini ya hatari na mwitikio wa dharura za kiafya.
Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna upungufu wa fedha za utafiti, mifumo ya ufuatiliaji isiyo imara na udhaifu katika mifumo ya tahadhari za mapema.
WHO imezitaka serikali za Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani katika sayansi na ubunifu, huku ikiwahimiza washirika wa kimataifa kuunga mkono juhudi zinazoongozwa na Afrika kwa usawa na kuongeza upatikanaji wa teknolojia na maarifa.
“Ubunifu wa kisayansi unapaswa kuwafikia wote. Ugunduzi ambao hauwafikii wanaouhitaji zaidi bado ni kazi ambayo haijakamilika,” amesisitiza Dk Janabi.
