Simulizi ya Shemndolwa aliyemaliza kifungo na maisha mapya ya ufundi

Njombe. Miaka 15 iliyopita, Rashid Shemndolwa maarufu Zunde aliingia gerezani akiwa kijana wa miaka 22, akiwa na ndoto zilizokatizwa na hukumu ya kifungo kirefu.

Baada ya kutumikia adhabu hiyo, anatoka nje ya kuta za gereza akiwa mtu tofauti akiwa na ujuzi wa ufundi uashi, cheti cha taaluma na zana za kazi mkononi tayari kuanza maisha mapya.

Shemndolwa (37), mzaliwa wa Mkoa wa Tanga, ni miongoni mwa wafungwa waliopata fursa ya mafunzo ya ufundi wakiwa gerezani, hatua iliyobadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yake.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi Aprili 7, 2026, amesema kabla ya kuhukumiwa kifungo hicho alikuwa akiendesha bodaboda mkoani Tanga bila kuwa na ujuzi wowote wa taaluma ya ufundi.

Lakini akiwa gerezani, aliona tangazo la fursa ya wafungwa kujiunga na mafunzo ya ufundi na yeye hakusita kuitumia nafasi hiyo.

“Nikiwa natumikia kifungo changu nilipata nafasi ya kwenda kusoma ufundi ujenzi. Niliamua kuitumia vizuri kwa sababu nilijua siku moja nitarudi uraiani,” amesema.

Alijiunga na mafunzo ya ufundi uashi yaliyotolewa katika Chuo cha Ufundi cha Magereza Ruanda kilichopo Mbeya, kozi iliyochukua miezi sita.

Baada ya kumaliza mafunzo hayo alifanikiwa kuhitimu na kupatiwa cheti cha taaluma huku akiendelea kutumikia kifungo chake.

Shemndolwa amesema aliingia gerezani kwa kosa la shambulio na kuhukumiwa kifungo cha miaka 15, akipewa namba ya mfungwa 86/2024.

“Niliingia gerezani kwa kosa la shambulio au udhalilishaji, nilianzia kifungo change Maweni Tanga kabla ya kuhamishiwa katika Gereza la Kilimo Ludewa mkoani Njombe.Huko nilianza safari ya kujifunza ufundi ambayo leo inanipa matumaini mapya ya maisha,” amesema Shemndolwa.

Amesema makosa yaliyomfikisha gerezani hayatakuwa sehemu ya maisha yake tena, akieleza kuwa elimu na mafunzo aliyoyapata yamembadilisha mtazamo kuhusu maisha.

“Mafunzo niliyoyapata yamenifundisha nidhamu, kazi na kuishi vizuri na jamii. Nina uhakika sitarudi tena gerezani,” amesema Shemndolwe katika mahojiano hayo.

Baada ya kumaliza kifungo chake, Shemndolwa alipatiwa zana za ufundi zenye thamani ya Sh1.5 milioni ili zimsaidie kuanza shughuli za ujenzi kama chanzo cha kipato.

Akimshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, amesema msaada huo utakuwa mtaji wa kuanza maisha mapya.

“Ninashukuru kwa vifaa hivi. Vitaniwezesha kuanza kazi na kujitegemea. Nimejifunza kwamba hata gerezani kuna nafasi ya kujenga maisha mapya,” alisema.

Shemndolwe hakusita kutoa wito kwa vijana kuepuka kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuwapeleka gerezani, akisema licha ya yeye kupata fursa ya kujifunza, si mahali salama kwa mtu yeyote.

“Vijana wajiepushe na makosa. Gereza siyo mahali pazuri isipokuwa kwa wale wanaotaka kujifunza na kubadilika,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Njombe, Joseph Mkude, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Magereza Tanzania, Jeremiah Katungu, amesema Shemndolwa alipata nafasi ya kumuomba msaada wa zana za kazi wakati wa ziara ya kiongozi huyo mkoani humo.

Mkude amesema baada ya kusikiliza maombi yake, Mkuu wa Magereza aliahidi kumsaidia ili aweze kuanza maisha mapya baada ya kumaliza kifungo.

Amesema mafunzo aliyoyapata Shemndolwa yalitolewa kupitia Chuo cha Ufundi cha Magereza Ruanda Mbeya kilicho chini ya usimamizi wa Veta.

“Alipata mafunzo ya miezi sita ya ufundi uashi na kufaulu vizuri katika nadharia na vitendo,” amesema Mkude.

Baada ya kuhitimu, Shemndolwa alipelekwa Gereza la Njombe kushiriki katika shughuli za ujenzi kama sehemu ya kuendeleza ujuzi wake.

Mkuu wa Magereza Wilaya ya Njombe, Jamhuri Njaidi, amesema mfungwa huyo alitoa mchango mkubwa katika miradi ya ujenzi inayotekelezwa na jeshi la magereza mkoani humo.

“Alishiriki katika ujenzi wa miundombinu ya miradi ya kiuchumi ya jeshi la magereza. Ni mfano kwamba mtu anaweza kubadilika na kuwa na manufaa kwa jamii,” amesema Njaidi.

Hata hivyo, ameiomba jamii kumpokea na kumuamini kama raia mwingine yeyote anayerejea katika maisha ya kawaida.

Baadhi ya vijana mkoani Njombe akiwemo Faraja Lugome wamelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutoa fursa za mafunzo ya ufundi kwa wafungwa, wakisema hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza vitendo vya uhalifu baada ya wafungwa kumaliza vifungo vyao.

“Wafungwa wanapopata ujuzi wanakuwa na kitu cha kufanya wanapotoka gerezani. Hii inaweza kusaidia kupunguza uhalifu katika jamii,” amesema Lugome.