Uchafu wazua taharuki mnada wa Maswa, wafanyabiashara walalamika

Maswa. Malalamiko ya wafanyabiashara na wananchi yameongezeka katika Mnada wa Maswa Mjini baada ya marundo ya taka kuonekana yakikaa kwa muda mrefu bila kuondolewa, hali inayodaiwa kuhatarisha afya za watu na kuharibu mazingira ya biashara katika eneo hilo.

Licha ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kumpa mzabuni jukumu la ukusanyaji na uondoaji wa taka, wafanyabiashara wanasema huduma hiyo haitekelezwi ipasavyo, jambo linalosababisha uchafu kuendelea kurundikana katika maeneo ya biashara.

Ziara ya Mwananchi katika mnada huo uliopo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa imekuta marundo ya taka yakiwa yamewekwa pembezoni mwa mnada na karibu na vibanda vya wafanyabiashara, huku baadhi ya maeneo yakitoa harufu kali.

Wakizungumza Aprili 7, 2026, baadhi ya wafanyabiashara walisema tatizo hilo limekuwa likijirudia mara kwa mara huku wakilalamikia kile wanachodai ni ukosefu wa ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa mamlaka husika.

Sehemu ya rundo za takataka katika eneo la mnada mjini Maswa. Picha na Samwel Mwanga

Agnes Tungu, ambaye ni mamalishe katika mnada huo, alisema licha ya taka kukusanywa mara kwa mara, huachwa kwa siku kadhaa bila kuondolewa.

“Mara nyingi taka zinakusanywa lakini zinakaa hapa kwa siku nyingi bila kuondolewa. Hali hii si nzuri kwa afya zetu wala kwa wateja wanaokuja kununua bidhaa,” amesema Agnes.

Naye Japhet Joseph ambaye ni mfanyabiashara wa dagaa katika mnada huo, amesema kinachowashangaza ni kuona mazingira yakiwa machafu wakati wafanyabiashara wanaendelea kulipa ushuru wa kila siku unaojumuisha pia tozo za usafi wa mazingira.

“Hapa ushuru unakusanywa kila siku, lakini mazingira hayako safi. Tunajiuliza fedha hizi zinaenda wapi kama huduma ya msingi kama usafi inashindwa kutekelezwa ipasavyo,” amesema Japhet.

Kwa upande wake, mkazi wa Mtaa wa Unyanyembe mjini Maswa, Said Yusuph, ameiomba Serikali na mamlaka za mji huo kuchukua hatua za haraka kuhakikisha taka zinazokusanywa zinaondolewa kwa wakati.

“Ni muhimu halmashauri na mamlaka ya mji mdogo kuhakikisha taka zinazokusanywa zinaondolewa kwa wakati ili kulinda afya za wananchi na kuboresha mazingira ya biashara,” amesema Said.

Takataka za maganda ya miwa zikiwa zimerundikwa katika eneo la mnada mjini Maswa lakini bado hazijaondolewa. Picha na Samwel Mwanga

Akizungumzia athari za kiafya zinazoweza kujitokeza, mtaalamu wa afya ya mazingira, James Kato, amesema taka zinapoachwa kwa muda mrefu zinaweza kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko.

“Kuachwa kwa taka kwa muda mrefu kunaweza kusababisha kuenea kwa magonjwa kama kipindupindu, kuhara na pia kuvutia wadudu waharibifu kama nzi na panya,” amesema Kato.

Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa, Caroline Shayo amesema ni kweli mzabuni wa ukusanyaji taka yupo lakini bado kuna changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema kwa sasa mamlaka hiyo inaendelea kufanya tathmini ili kubaini changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua ili kuhakikisha mji wa Maswa unakuwa safi.

“Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa tuna jukumu la kuhakikisha mji unakuwa safi. Tutamsimamia mzabuni kuhakikisha anatekeleza kikamilifu majukumu yote yaliyoainishwa katika mkataba wake na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,” amesema Shayo.