Barker ang’ara, Imoro aibuka mchezaji bora Ligi Kuu NBC Machi

Kocha wa Simba SC, Steve Barker, amechaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 baada ya kuiongoza timu yake kupata matokeo chanya.

Barker aliiwezesha Simba kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi. Katika kinyang’anyiro hicho, aliwashinda Pedro Goncalves wa Young Africans SC na David Ouma.

Katika tuzo za wachezaji, beki wa Singida Black Stars, Ibrahim Imoro, ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Machi baada ya kuonesha kiwango bora katika michezo mitano, akifunga mabao matatu na kuisaidia timu yake kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya sita kwenye msimamo wa ligi.

Imoro aliwashinda Anicet Oura wa Simba SC pamoja na Lamine Jarjou katika fainali za tuzo hizo zilizoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.

Katika tuzo nyingine, Meneja wa Airtel Stadium, Omar Malule, amechaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Machi kutokana na ubora wake katika usimamizi wa matukio ya michezo pamoja na miundombinu ya uwanja.

Kwa upande wa Ligi ya NBC Championship, Omari Mponda wa Mbuni FC ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi huo baada ya kufunga mabao mawili ndani ya dakika 155 za michezo miwili aliyocheza. Aliwashinda Yusuf Mhilu na Maulid Shaaban.

Naye Zuberi Katwila wa Geita Gold FC amechaguliwa Kocha Bora wa mwezi Machi wa Championship baada ya kuiongoza timu yake kushinda michezo yote miwili na kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi, akiwashinda Leonard Budeba na Twaha Beimbaya.

Aidha, Kamati ya Tuzo ya TFF imetaja mabao matatu yatakayowania tuzo ya Bao Bora la Mashabiki kwa mwezi Machi. Magoli hayo ni ya Prince Dube (Yanga v Singida BS), Joseph Akandwanaho (TRA v Namungo) pamoja na Ibrahim Imoro (Singida BS v Mbeya City).

Mashabiki wanatarajiwa kushiriki kupiga kura ili kumpata mshindi wa tuzo hiyo maalum ya bao bora.