Global Publishers
April 8, 2026
0 Comments
Tamasha kubwa la muziki la Wireless Festival limefutwa rasmi baada ya Rapa Ye (zamani akijulikana kama Kanye West) kuzuiwa kuingia nchini Uingereza kufuatia historia ya kauli zake za chuki dhidi ya Wayahudi.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali ya Uingereza kumkatalia Ye kibali cha kuingia nchini, ikisema uwepo wake hauwezi kuwa “kwa manufaa ya umma.” Waziri Mkuu Keir Starmer alisisitiza kuwa serikali yake haitavumilia chuki ya aina yoyote, akieleza wazi msimamo dhidi ya antisemitism.

Tamasha hilo lilipangwa kufanyika Julai 10–12 katika Finsbury Park jijini London, likitarajiwa kuvutia zaidi ya mashabiki 150,000. Hata hivyo, baada ya msanii huyo kuzuiwa, waandaaji walilazimika kulifuta kabisa na kuahidi kurejesha fedha za tiketi kwa mashabiki.
Shinikizo kubwa lilitoka kwa wadhamini wakubwa kama Pepsi, Rockstar Energy na Diageo ambao walijiondoa mara tu Ye alipotangazwa kuwa msanii mkuu.
Kwa muda mrefu, Ye amekuwa akikosolewa kutokana na matamshi yake ya chuki na hata kuonyesha wazi kuvutiwa na Adolf Hitler jambo lililosababisha upinzani mkali kutoka kwa jamii ya Wayahudi na viongozi wa kisiasa.
Ingawa rapper huyo aliomba radhi mapema mwaka huu na kusema yuko tayari kukutana na jamii ya Wayahudi ili kujifunza na kubadilika, viongozi wa jamii hiyo wamesisitiza kuwa toba ya kweli lazima ionekane kwa vitendo kabla ya kurejeshwa kwenye majukwaa makubwa kama tamasha hilo.
Kwa kifupi, kufutwa kwa Wireless Festival ni pigo kubwa kwa mashabiki wa muziki Uingereza, lakini pia ni ishara ya msimamo mkali unaochukuliwa dhidi ya chuki na matamshi yenye kuumiza jamii.