Kichanga wa miezi tisa aokotwa jalalani Mbozi

Songwe. Wakazi wa Mtaa wa Msaki, Kata ya Ichenjezya, wilayani Mbozi mkoani Songwe, wamekumbwa na taharuki baada ya mwili wa mtoto mchanga wa kike, anayekadiriwa kuwa na miezi tisa, kupatikana ukiwa ndani ya bahasha na kutupwa kwenye dampo la takataka lililopo mtaani hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini na kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria mhusika wa kitendo hicho, ambacho amesisitiza hakikubaliki katika jamii.

Amesema mwili wa mtoto huyo umepelekwa katika Hospitali ya Mbozi kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu, huku juhudi za kumtafuta mama wa mtoto huyo zikiendelea.

Aidha, amekemea vitendo vya aina hiyo, akisisitiza kuwa endapo kuna changamoto kama kukataliwa na mwanaume au matatizo ya kijamii, wahusika wanapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka husika badala ya kuchukua hatua za kikatili zinazohatarisha maisha ya watoto.

Pia, mashuhuda wa tukio hilo, wakiwemo wafanyakazi wa usafi wanaokusanya taka katika eneo hilo, wamesema mwili wa kichanga hicho uligundulika asubuhi ya Aprili 7, 2026 ukiwa umefungwa ndani ya bahasha kubwa na kutupwa damponi.

Wamesema mwili huo ulikuwa umeanza kuharibika, hali inayodaiwa kusababishwa na kunyeshewa na mvua baada ya kutupwa eneo hilo.

Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Vwawa na shuhuda wa tukio hilo, Petro Kayange amesema matukio ya kutupa watoto wachanga katika dampo hilo yamekuwa yakijirudia.

Kayange amesema hili ni tukio la pili kushuhudiwa katika eneo hilo, ambapo awali pia walikuta kichanga kikiwa kimetupwa ndani ya bahasha, hali inayozua sintofahamu na maswali mengi miongoni mwa wakazi.

“Hatuyakuti matukio mengine kwenye madampo ni hili tu kwani mara ya kwanza tulimkuta mtoto jinsia ya kiume tunaomba ushirikiano baina ya wananchi na Jeshi la Polisi ili kuwakamata wahusika wanaotupa watoto,” amesema Kayange.

Joseph Waraha amesema wamemkuta mtoto huyo akiwa bila nguo kwani alikuwa amewekwa kwenye bahasha ambayo ililowa baada ya mvua kunyesha usiku kucha na wakati tukiendelea na kuzoa taka tulibaini mwili wa kichanga kikiwa kimeaharibika.

“Nawaomba sana wanawake kuacha matukio ya ukatili dhidi ya watoto wanapozaa, kwani kama mimba wamelea miezi tisa, cha kujiuliza kwa nini utupe kiumbe kilichozaliwa? amehoji Waraha.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Masaki lilipo dampo hiloi Sifa Nassor amesema hilo ni tukio la pili kutokea katika dampo hilo huku akiomba mamlaka kufanya utaratibu wa kulihamisha kwani lipo jirani na makazi na uzoaji wa taka umekuwa ukichelewa na kuhatarisha afya zao.

“Tunaomba ushirikiano kwa wananchi kutoa taarifa kwa ndugu yake au jirani yake aliyekuwa mjamzito na sasa hana mtoto ili aweze kukamatwa na hatua zingine za kisheria zichukuliwe,” amesema Nassoro.