Latra yaongeza siku 14 kupokea maoni mapitio ya nauli mpya

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) imeongeza wiki mbili zaidi za kupokea maoni kutoka kwa wadau wa usafirishaji kuhusu mapitio ya nauli baada ya upandaji wa bei za mafuta ulioanza Aprili mosi, 2026.

Aprili mosi, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza ongezeko hilo la bei za mafuta, linaloelezwa kuchochewa na mgogoro wa kimataifa unaoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ulioanza Februari 28, 2026.

Mgogoro huo umeathiri uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ghafi duniani, hasa baada ya kufungwa kwa mlango wa Hormuz, ambao hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani.

Vilevile, kushambuliwa kwa visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na viwanda vya kuyasafisha kumeigusa moja kwa moja Tanzania, ambayo inaagiza mafuta kwa kiasi kikubwa, jambo linalotajwa kuongeza gharama za usafirishaji kutokana na kukosekana kwa meli za kuyasafirisha.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Dk Habibu Suluo, taarifa za leo zinaonesha bei ya mafuta imeshuka, hivyo baada ya mchakato wa kupokea maoni kukamilika, watapata picha ya hali inavyokwenda.

Dk Suluo ameeleza hayo leo, Jumatano, Aprili 8, 2026, wakati wa kikao kilichoandaliwa na taasisi hiyo kupokea maoni ya wadau wa usafirishaji baada ya gharama za mafuta kupanda kuanzia Aprili mosi, 2026.

Bosi huyo wa Latra amesema hata baada ya kikao hicho cha wadau kutamatika, wataendelea kupokea maoni hadi Aprili 21 ili kutoa fursa zaidi kwa wasiopata nafasi kuwasilisha mapendekezo yao kwa mfumo wa barua pepe.

Dk Suluo amefafanua kuwa kesho, Alhamisi, Aprili 9, 2026, kutakuwa na kikao cha juu cha Serikali kitakachofanyika jijini Dodoma, kitakachoangalia nini kifanyike ili huduma ziendelee.

Amefafanua kuwa licha ya changamoto zilizopo Mashariki ya Kati na juhudi za kimataifa zinazoendelea kushughulikia hali hiyo, ikiwemo athari za migogoro ya kimataifa, Tanzania haiwezi kusubiri bila kuchukua hatua.

“Leo hatuna majibu, tunawasikiliza, maana ninyi ndio mpo kwenye uwanja wa kazi ili biashara zenu zisife. Ni lazima tupokee maoni yenu na tuangalie mchakato utakuwa vipi, hususan kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri na wafanyakazi katika sekta hii,” amesema.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Barabara wa Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana, amesema Serikali ipo kwa ajili ya kusikia na kuchambua ili kupata uelewa wa pamoja wa kitu gani kifanyike.

“Kupitia majadiliano haya, tutatoka na mwelekeo utakaolinda maslahi ya mtoa huduma, mtumia huduma na uchumi wa Taifa,” ameeleza Magombana.