Maswa. Wananchi wilayani Maswa mkoani Simiyu wameiomba Serikali kuongeza juhudi za utoaji wa elimu ya lishe katika ngazi ya jamii, ili kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto ambalo bado linaendelea kuathiri familia nyingi.
Wakizungumza Aprili 8, 2026, baadhi ya wananchi wamesema kuwa licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wa afya, bado uelewa kuhusu lishe bora ni mdogo, hasa katika maeneo ya vijijini.
Mkazi wa kijiji cha Mwabayanda ‘M’, Felister Mhoja, amesema wazazi wengi hawana maarifa ya kutosha kuhusu aina sahihi ya vyakula vinavyohitajika kwa ukuaji wa mtoto.
“Watu wengi wanajua kumpa mtoto ugali na mboga pekee, lakini hawatambui umuhimu wa vyakula kama mayai, maziwa na matunda katika ukuaji wa mtoto,” amesema.
Kwa upande wake, Mwanahawa Ally wa Kata ya Lalago amesema changamoto si upatikanaji wa chakula, bali ni ukosefu wa elimu ya namna ya kuandaa mlo kamili.
“Tunazalisha mazao mbalimbali, lakini hatujui jinsi ya kuyachanganya ili mtoto apate lishe bora. Elimu zaidi inahitajika,” amesema.
Naye mkazi wa mjini Maswa, Elisha Ndalo, amesisitiza umuhimu wa utoaji wa elimu ya lishe mara kwa mara kupitia vituo vya afya na mikutano ya kijiji, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kubadili mtazamo wa wazazi wengi.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano. Picha na Samwel Mwanga
Akizungumzia hali hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kupambana na udumavu, ikiwemo utoaji wa elimu ya lishe kupitia vituo vya afya, kliniki za watoto na kampeni za afya.
Amefafanua kuwa udumavu kwa watoto mara nyingi husababishwa na ukosefu wa lishe bora katika miaka ya mwanzo ya maisha, na kusisitiza umuhimu wa wazazi kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili unaojumuisha vyakula vya aina mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wataalamu wa afya pamoja na viongozi wa ngazi za chini ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.
“Tutaimarisha utoaji wa elimu ya lishe kupitia mikutano ya vijiji na taasisi mbalimbali ili kupunguza tatizo la udumavu, ambalo kwa sasa linafikia asilimia 32 katika wilaya yetu,” amesema.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa wazazi, viongozi wa jamii na wataalamu wa afya ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora itakayochangia ukuaji wao wa mwili na akili.
