Mbio za Dola 150,000 zaanza rasmi Dar City ikianza maandalizi

Timu ya mpira wa kikapu ya Dar City itaanza maandalizi ya kuziwinda Dola 150,000  (Sh388.2m) na ubingwa wa Afrika (BAL) Aprili 17.

Mpaka sasa, Dar City imejihakikishia kitita cha Dola za Kimarekani 70,000 (Sh181.2m) kwa kufuzu hatua ya 12 bora ya mashindano ya BAL yaliyomalizika hivi karibuni mjini Pretoria, Afrika Kusini na kumaliza katika nafasi ya nne.

Endapo Dar City itashinda hatua ya finali iliyopangwa kufanyika mjini Kigali, Rwanda kuanzia Mei 22 mpaka 31 itazawadiwa jumla ya Dola za Kimarekani 220,000, ikiwa Dola za Kimarekani 70,000 za kufuzu hatua hiyo na Dola 150,000 za ubingwa.

Meneja Mkuu wa Dar City, Simon Mirondo amesema kuwa kwa sasa wachezaji wamepewa mapumziko ya siku 10 na watatakiwa kuanza mazoezi Aprili 17.

Alisema kuwa baadhi ya wachezaji wazawa, wataanza mazoezi hayo huku wale wa kigeni wataanza kwa kadri siku zinavyokwenda.

“Kwa sasa wachezaji wetu wapo mapumziko ya siku 10. Mazoezi yakayoaanza yatakuwa ya wachezaji wazawa, huku wale wa kigeni ambao kwa sasa wapo nje ya nchi watajiunga kwa kadri ya maelekezo.

Kambi ya sasa itafanyikia Dar es Salaam baadala ya Zanzibar kama ilivyokuwa awali,” alisema Mirondo.

Alisema kuwa mashindano ya Kigali yatakuwa magumu kwani yanashirikisha timu ambazo zimefuzu hatua ya mchujo wa timu 12.

Mbali ya Dar City, timu nyingine kutoka kundi la Kalahari ni  RSSB Tigers (Rwanda), Petro de Luanda (Angola) na Al Ahly Ly ya Libya.

Timu hizo zitaungana na timu  nne kutoka kundi la Sahara ambazo wataanza mashindano ya mchujo kuanzia Aprili 24 mpaka Mei 3 kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat, Morocco.

Timu hizo ni Al Ahly (Misri), ASC Ville de Dakar (Senegali), Club Africain (Tunisia), FUS Rabat (Morocco),  JCA Kings (Ivory Coast) na Maktown Flyers ya Nigeria.

“Kwa mujibu wa taratibu, tunatakiwa kuongeza nguvu kwa usajili wa mchezaji mmoja. Kwa sasa tuna wachezaji wawili ambao wanauguza majeraha ambao ni David Michineau na Michael Foster. Taarifa za madakatari wetu ndizo zitaamua hatma yao,” alisema.