Dodoma. Mbunge wa Monduli (CCM), Isack Capriano ameiomba Serikali itafakari njia bora ya kuwasaidia madiwani kwa kuongeza posho zao, akieleza kuwa kiwango cha sasa hakikidhi mahitaji yao.
Capriano ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Aprili 8, 2026, wakati akichangia hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu bajeti ya mwaka 2026/27.
Amesema kuwa kiwango cha Sh350,000 wanachopata madiwani ni kidogo na kinawafanya waishi maisha magumu.
Amesema kuwa kazi kubwa wanazofanya madiwani haziendani na kiwango hicho cha posho, hivyo ameomba Serikali iruhusu halmashauri kutumia mapato yao ya ndani kuongeza posho za madiwani, ambazo kwa sasa zinalipwa na Hazina.
“Mimi nimekuwa diwani kwa miaka 15, nayajua maisha ya madiwani namna yanavyobeba mazingira magumu na wakati mwingine wanatumia akiba zao mifuko kuwasaidia wananchi, naomba Serikali iruhusu mapato ya ndani walau kila halmashauri iweze kuweka nyongeza ya Sh150,000 ili diwani alipwe Sh500,000 walau inaweza kusaidia,” amesema Capriano.
Hoja ya mbunge huyo inaungana na ile iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Mbunge wa Chemba (CCM), Kunti Majala, aliyesema kuwa kutoongezwa kwa posho za madiwani kunadhoofisha utendaji kazi na usimamizi wa rasilimali katika halmashauri.
Hata katika Bunge la 12, iliibuliwa hoja ya kuongeza posho za madiwani, jambo ambalo lilichukua muda mrefu kuzungumzwa, huku kuelezwa kuwa Serikali ilikuwa inalifanyia kazi.
Katika hatua nyingine, leo Capriano ameitaka Serikali kusimamia ipasavyo matamko yake, akisisitiza kuwa yanapobaki kwenye makaratasi hupoteza maana na kuwafanya baadhi ya watu kuonekana wako juu ya sheria.
Alitoa kauli hiyo akirejea tamko la Waziri Mkuu lililotolewa wakati wa mkutano wa pili wa Bunge la 13, ambapo alieleza kuwa vikao vya kamati za halmashauri vitaandaliwa kwa kuzingatia ratiba za Bunge, hususan kufanyika siku za Jumamosi ili kuwawezesha wabunge kushiriki.
“Haya mambo tuangalie ili yasibaki kwenye makaratasi, muda huu mimi ndiyo nimepokea ratiba ya kikao cha fedha sijui kinafanyika jumatano na siku gani wakati mimi nipo bungeni hapa, mkitoa matamko na kauli muwe mnafuatilia utekelezaji wake,”amesema Capriano.
